Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, DODOMA
RAIS Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwathamini wawekezaji kwa kuridhia kupunguzwa na kufutwa baadhi ya tozo zilizokuwa zikitozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) zenye thamani ya Sh.Bilioni 35.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wakati wakipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya OSHA.
Amesema hatua hiyo ilitokana na ombi la wafanyabiashara kupitia Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) ili kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji nchini.
Katambi amesema masuala ya usalama na afya mahali pa kazi yataendelea kupewa uzito na serikali ili kuhakikisha nguvu kazi iliyopo inakuwa salama.
Naye, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema tozo ya upimaji umeme katika vituo vya mafuta hasa maeneo ya vijijini imepunguzwa kutoka Sh.650,000 hadi Sh.150,000 ili kuvutia wawekezaji na kuondokana na mafuta kuuzwa kwenye chupa.
Amesema kumekuwapo na matokeo chanja ambapo OSHA imevifikia vituo 2,708 ikilinganishwa na kabla ya kupunguzwa tozo vilifikiwa vituo 1,153.
Kadhalika, amesema kutokana na Tanzania kutekeleza kwa kiwango kikubwa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi imekuwa mfano kwa mataifa mengine kuja kujifunza.
Akihitimisha kikao cha kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq amepongeza serikali kwa kuendelea kufanyia kazi maoni ya kamati ya kuimarisha masuala ya usalama mahali pa kazi kwa kuipatia OSHA vitendea kazi ili itekeleze majuku yake kwa ufanisi zaidi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba