Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Tanga
ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Sonia Magogo, ajiunga na CCM, huku akisema kazi kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uongozi wake zimemsukuma kukihama chama chake cha zamani.
“Rais Samia anafanyakazi kubwa, ni Mama aliyejaa busara ,ni mama anayejali na ni mama anayeipenda nchi yake. Na hiyo imemsukuma kujiunga na CCM ili kuongeza nguvu kuhakikisha Tanzania inasonga mbele,” alisema Magogo.
Magogo ametangaza uamuzi huo kwenye mkutano wa CCM uliofanyika wilayani Handeni juzi na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah Abdurahman.
Aidha, alisema kwa namna ya pekee anampongeza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga (Abdurahman) kwa namna ambavyo amekuwa akikimbia kwenye mkoa mzima wa Tanga kutumikia wananchi.
Alisema hilo, nalo limemvutia na ana imani na viongozi wote wa CCM Mkoa wa Tanga hadi leo CCM inaendelea kushamiri mkoani humo.
Magogo amesema ameona hakuna sababu ya kuendelea kuvutana, kwani kinachohitajika ni maendeleo ikiwemo kuhakikisha Mkoa wa Tanga unapiga hatua.
“Hivyo hatuna muda wa kuendelea kuvutana kwa pamoja tunaweza na ninawaahidi ushirikiano wa hali ya juu. Kuna yale ambayo nadhani ninayo, tutayapokea kwa maslahi ya Hadeni, Chama na Taifa kwa ujumla,” amesema Magogo.
Amesema anahitaji ushirikiano wao na ana mawazo anaomba wayapokee kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Alisema maamuzi ya kuhamia CCM hakuyafanya peke yake, ana wenzake ambao wameandamana pamoja katika hilo ambao ni pamoja na aliyekuwa mwekiti wa umoja wa vijana CUF.
Magogo alikuwa mbunge wa viti maalum CUF mkoa wa Tanga kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 na katika uchaguzi wa mwaka 2020 aligombea ubunge Jimbo la Handeni, ambapo hakushinda katika uchaguzi.
Magogo amekuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kwenye siasa za Mkoa wa Tanga, ambapo uamuzi wa kujiunga na CCM utaisaidia kuimarisha chama hicho.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba