January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kasi ya Rais Samia kufungua uchumi iwaamshe wasaidizi

Na Markus Mpangala, TimesMajira Online

UTAFITI Oxford Economics mwaka 2016 unaonesha kuwa asilimia sabini na nane(78%) ya biashara ya bidhaa na huduma imefungamanishwa na rasilimali za asili za nchi za kusini kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia ya mahusiano kati ya biashara moja na nyingine, nchi moja na nyingine au kampuni moja na nyingine.

Nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zinachangia asilimia arobaini na saba (47%) ya hiyo asilimia sitini kwa njia ya moja kwa moja au njia ya mahusiano ya kibiashara.

 Pamoja na kujifungamanisha na biashara hii ya Dunia kiasi hicho, bado mchango wa Afrika, kusini mwa Sahara kwenye biashara ya dunia, ni chini ya asilimia nne nukta tano (4.5) kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni za Chuo Kikuu cha Sussex cha nchini.

Kwa msingi bado safari ya kufungua uchumi ingalipo na serikali inafanya juhudi kuhakikisha kila mkoa wa Tanzania unatumia fursa zake kuinuka kiuchumi. Uthibitisho wa safari ya Rais Samia kufungua uchumi wa mikoa ya kusini na namna anavyoiunganisha na sehemu nyingine.

Inafahamika kuwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika wilaya ya Tunduru kuunganisha na wakazi wan chi ya Msumbiji ni lango mojawapo la kuifungua nchi yetu kiuchumi.

Vilevile wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanayo matumaini makubwa baada ya serikali kuendelea kumpa nafasi mkandarasi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kitai hadi Ruanda ambako eneo hilo limekuwa likitawaliwa na wawekezaji wakubwa wanaochimba Makaa ya Mawe.

Vitalu vya uchimbaji wa Makaa ya Mawe kuanzia kijiji cha Amanimakoro hadi Ruanda vinatarajiwa kufungua uchumi wa wananchi wa mikoa ya kusini na kujiunganisha na majirani zao wa Msumbiji, Malawi na hata Zambia.

Meli za abiria kutoka Msumbiji zinatarajiwa kufanya safari upande wa bandari za Tanzania jambo ambalo limekuza uhusiano mkubwa unaoendelea kwa sasa kutokana na juhudi za serikali ya awamu ya sita.