Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
KUKOSEKANA kwa upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania imetajwa kuwa moja ya chanzo cha mauaji ambayo yametokea katika maeneo mengi hapa nchini katika siku za hivi karibuni.
Sababu hiyo imetajwa juzi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ongezeko la matukio ya mauaji ambayo yametokea hivi karibuni katika maeneo mengi hapa nchini.
Mgeja alisema katika uchunguzi wake amebaini matukio mengi ya mauaji ni hayo yanayohusiana na wivu wa kimapenzi kati ya wapendanao na uwaniaji wa mali ndani ya familia, ambapo baadhi ya watoto wamekuwa wakiwaua wazazi wao kwa lengo la kupata mali.
Akifafanua zaidi alisema ukichunguza kwa undani ni wazi kwamba mauaji hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na watu kutokuwa na upendo miongoni mwao, hasa ikizingatiwa wanaofanya mauaji hayo ni watu wa karibu kabisa ndani ya familia.
Alisema iwapo Watanzania watadumisha upendo na mshikamano miongoni mwao kama walivyo viumbe wengine mfano wa ndege aina ya njiwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya mauaji yanayotokea hivi sasa hapa nchini.
“Watanzania tudumishe upendo na mshikamano kama walivyo viumbe wengine mfano wa ndege aina ya njiwa, maana tusipokuwa na upendo ni wazi tunaweza kutoana roho kwa mambo madogo madogo ambayo kama upendo na mshikamano vingekuwepo yasingetokea,”
“Nichukue fursa hii kuwaomba Watanzania wenzangu, tujenge utamaduni wa kupendana na kuhurumiana pale mmoja wetu anapopatwa na matatizo asaidiwe badala ya kuchekwa, na kama ni suala la mahusiano ya kimapenzi, basi busara itumike katika kutatua changamoto zinazojitokeza, badala ya kukimbilia kutoana roho,” alisema Mgeja.
Mgeja alitoa mfano wake yeye mwenyewe ambaye amekuwa na tabia ya kuwakirimu kwa kuwapa chakula ndege aina ya njiwa ambao kwa kipindi kirefu na wao wameonesha upendo kwake kutokana na kwenda nyumbani kwake kila asubuhi na kukaa naye pamoja japokuwa wao si binadamu wenzake.
“Ukiacha wanadamu hata kama tutawakirimu viumbe wengine katika kuwapa sadaka na kuwafanyia hisani, kuwahurumia na kuwathamini pia na wao wana nafasi kubwa ya kutuombea mbele ya muumba wetu ili tuishi kwa amani na upendo”
“Hali ya upendo ikidumishwa na kujenga utamaduni wa kuhurumiana nchi yetu ama miji yetu itaendelea kuwa na amani na upendo ndani mwetu, mfano ni hawa njiwa, mimi siwafugi, lakini huja hapa kila siku asubuhi, kisha wanaondoka, hii wanaonesha jinsi gani binadamu tunapaswa kupendana,” alieleza Mgeja.
Kutokana na hali hiyo Mgeja amewaomba viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini katika ibada na maombi yao ya kila siku wahimize sana suala la waumini wao kuwa na upendo na waone madhara ya kuuana wao kwa wao kwa mambo madogo madogo ya kidunia kwa vile hapa duniani ni mapito tu.
“Niwaombe watanzania wenzangu, tumrejee muumba wetu bila kujali tofauti zetu za kidini, ukabila, kisiasa ama kijinsia, tukumbuke sisi sote ni ndugu, hatuna sababu za kuuana kwa suala la kutaka urithi ama wivu wa kimapenzi, tuisaidie Serikali yetu kwa kuishi kwa amani na upendo ili tupate maendeleo tarajiwa,” alieleza Mgeja.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi