January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga: Hali ya uzalishaji umeme ipo vizuri

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kuwa hali ya uzalishaji umeme katika Kituo cha Kuzalisha umeme wa Megawati 43 unaotokana na gesi asilia kilichopo Tegeta, Dar es Salaam inaendelea vema na mitambo minne kati ya mitano iliyopo kituoni hapo inafanyakazi.

Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kukagua kituo hicho ambacho kinaendeshwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) amesema hali ya uzalishaji wa umeme katika kituo cha Tegeta ni nzuri, mitambo minne inafanya kazi, mmoja kati yao haufanyi kazi ambapo hadi sasa upo kwenye matengenezo na unakaribia kukamilika.

“Kikubwa ambacho nawaelekeza Tanesco ni kuhakikisha matengenezo ya mitambo yanafanyika kwa wakati na kwa muda mfupi ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini,” alisema na kuongeza

“Tanesco wanapaswa kuendelea kuimarisha huduma kwa wateja na kuzifanyia kazi kwa haraka kila hitilafu inapotokea ili umeme uendelee kupatikana,”amesema

Akizungumzia upatikanaji wa umeme majumbani

Amesema wanaendelea kufuatilia uzalishaji wa umeme kwa kiasi kikubwa na suala la kurudisha umeme kwa maeneo ambayo yamekatiwa umeme masaa 12 haitokubalika.”Itokee anazidishiwa muda wa kurudishiwa umeme urudishwe kwa wakati ili watu waendelee na shughuli za maendeleo,”alisema

Naibu Waziri Kapinga amesema wataendelea kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa umeme inaendelea kuimarika na kusimamia matengenezo kama walivyoagizwa na Rais Dtk. Samia Suluhu Hassan.

“Hatutakubali watanzania walale bila umeme kwa sababu ya changamoto ndogo ndogo ikiwemo kuharibika kwa Transfomer, mita, kukatika kwa wire ya umeme, naomba TANESCO mfatili kuhakikisha umeme unapatikana ndani ya muda mfupi” alisema Kapinga.

Kapinga amesema kuwa katika kituo cha kuzalisha umeme cha Tegeta Gas Plan uzalishaji wa umeme unaendelea kupitia mitambo mitano ambayo inazalisha megawatt 43.

Amesema kuwa kwa sasa mitambo minne inaendelea na uzalishaji wa umeme katika kituo cha Tegeta Gas Plan, huku akieleza kuwa mtambo mmoja mafundi wanaendelea matengenezo ya lazima.

“Lengo ni kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana, tutahakikisha kila mtanzania anapata umeme, hivyo wakati umefika kwa TANESCO kuunganisha umeme sehemu zote ambazo kuna miundombinu’’ amesema Kapinga

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Hanga, amesema kuwa TANESCO kwa kushirikana na Wizara ya Nishati inaendelea kufanya juhudi kadri inavyowezekana ili kuhakikisha umeme wa kutosha unapatikana kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kijamii na uzalishaji mali.
Alisema kuwa wanaendelea na jitihada mbalimbali ili kufikia malengo “Tunapokea kila aina ya ushauri ambao tunaona unaweza ukafaa, lengo umeme upatikane kwa gharama ambayo wananchi wanaweza kumudu.

Mhandisi Gissima Nyamo Hanga ameishukuru serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuhakikisha wanazalisha umeme wa kutosha.