📌 Ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika; Cha Kwanza kwa ukubwa EAC
📌 Kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku
📌 Ampongeza Dkt. Samia kutatua changamoto za wananchi kwa vitendo
📌 Aipongeza TPDC; Ataka Vituo vya CNG kuendelea kujengwa
Na Penina Malundo, Timesmajira
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amezindua Kituo Mama cha Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG) ambacho kina uwezo wa kujaza Gesi Asilia kwenye magari 1200 kwa siku huku kikifanya kazi kwa muda wa saa 24.
Kapinga amezindua kituo hicho tarehe 9 Mei, 2025 jijini Dar es Salaam akimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ambapo uzinduzi huo ulienda sambamba na uzinduzi wa basi la mfano la Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) ambalo litaendeshwa kwa kutumia nishati ya Gesi Asilia.
Akizungumza na halaiki iliyohudhuria hafla hiyo, Kapinga amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono, mtazamo na maelekezo yake kwa Wizara ya Nishati ambayo yanaleta matokeo chanya kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi kwa kituo hicho cha CNG.
Pia, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa uongozi wake ambao unapelekea upatikanaji wa nishati ya uhakika ambayo ni rafiki kwa mazingira na afya za wananchi.
“ Hapo nyuma kumekuwa na malalamiko ya uwepo wa foleni kubwa za ujazaji wa gesi kwenye vyombo vya moto katika vituo vya CNG ikiwemo kituo cha Ubungo Maziwa, lakini uwepo wa kituo hiki unaonyesha jinsi Serikali inavyotekeleza kwa vitendo ahadi inazotoa kwa wananchi za kupunguza kero ya upatikanaji wa CNG, nampongeza Rais Samia kwa kuendelea kutatua changamoto za wananchi na pia naipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa hatua hii.” Amesema Kapinga
Ameeleza kuwa, kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kujaza Gesi kwenye magari nane kwa wakati mmoja, kuchochea ongezeko la vituo vingine vya CNG na kuwapatia huduma ya gesi watumiaji wengine kama viwanda, shule, hoteli n.k
Kapinga ameiagiza TPDC kuhakikisha kuwa, kituo hicho kinakuwa mfano wa kutoa huduma bora na za viwango kwa wateja huku kikizingatia masuala ya usalama na utunzaji wa mazingira.

Pia ameiagiza TPDC kuendelea kujenga vituo vya CNG katika maeneo mengine ya nchi ikiwemo Lindi na Mtwara, pia kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi ili kuendelea kuchochea uwekezaji kwenye sekta ya CNG.
Naibu Waziri Kapinga pia ameishukuru Sekta binafsi kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya CNG.
Aidha, amewaasa Watanzania kuchangamkia fursa ya kuweka mifumo ya matumizi ya gesi kwenye magari yao kwani mifumo hiyo haiharibu magari hayo na pia watapata nafuu ya gharama za uendeshaji.
Kuhusu kampuni ya UDART ambayo kwa mara ya kwanza imezindua basi jipya linalotumia Gesi Asilia, ikiwa ni moja ya mabasi mengi yakayotumia gesi hiyo, Kapinga amesema kuwa ushirikiano kati ya TPDC na UDART utaendelea kuchochea uwekezaji kwenye CNG na kuendelea kuboresha huduma za usafiri jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameipongeza wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayofanyika ili kupata matokeo makubwa kwenye sekta na kuahidi ulinzi katika miundombinu hiyo ambayo ni muhimu katika kutoa huduma kwa wananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Kilumbe Ng’enda amesema Bunge limeridhishwa na hatua zinazochukuliwa kwa kasi na Serikali katika kuendeleza Sekta ya Gesi akieleza kuwa unapotumia gesi asilia kuendesha gari unapata unafuu kwa asilimia 40 ukilinganisha na mafuta.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameipongeza Bodi na Menejimenti ya TPDC kwa kutekeleza mradi huo kwa mafanikio, pia ameipongeza UDART ambao watakuwa wateja wakubwa wa CNG.
Amesema mradi huo ni wa kujivunia kwani kituo hicho kilichozinduliwa ni cha Pili kwa ukubwa barani Afrika na cha kwanza kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki

Mwenyekiti Bodi TPDC, Balozi Ombeni Sefue amesema Bodi na Menejimenti ya Taasisi hiyo itahakikisha changamoto ya wananchi kupanga foleni ndefu kwenye vituo vya CNG inaisha na watahakikisha rasilimali ya gesi asilia inapatikana wakati wote kupitia huduma mbalimbali ikiwemo ya kupikia na kuendeshea vyombo vya moto.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Francis Mwakapalila amesema kuwa katika kuchochea matumizi ya Gesi Asilia kwenye vyombo vya moto nchini, TPDC imeamua kuweka mkazo kwa kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujazia gesi asilia kwenye vyombo vya moto ikiwemo magari na bajaji kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa sasa tayari wameanza mchakato wa manunuzi ya vituo vitano vya CNG vinavyohamishika ambavyo vitawejwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Awali Mkurugenzi wa Idara ya Biashara ya Mafuta kutoka TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert alisema kuwa kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha CNG kiasi cha futi za ujazo milioni 4.2 sawa na kilo 120 kwa siku, kina pampu nne zenye jumla ya nozeli nane na hivyo kukifanya kituo kuwa na uwezo wa kuhudumia magari nane kwa wakati mmoja ambapo kwa siku kitatoa huduma kwa magari takriban 1200.
Ameongeza kuwa, kituo kina pampu maalum tatu kwa ajili ya kujaza magari maalum ya kusafirisha CNG kwenda kwenye vituo vidogo vya kujaza gesi kwenye magari (Offline CNG Filling Stations), viwandani, taasisi na majumbani.
More Stories
Madiwani Ilala walia na dampo la Pugu
TLS yaishauri serikali kuanzisha chombo maalumu
Ridhiwani ataka watu wenye ulemavu wapewe fursa