November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga aipongeza REA usambazaji Nishati Vijijini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa pongezi kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri ya kuendelea kusambaza umeme pamoja na aina nyingine za nishati vijijini ili kuhakikisha wananchi wote waishio vijijini wanafikiwa na huduma hiyo na kuboresha maisha yao.

Kapinga ametoa pongezi hizo Novemba 7, mwaka huu wakati akizungumza na Menejimenti ya REA, ikiwa ni kikao chake cha kwanza na Uongozi wa Wakala hiyo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

“Kazi ya REA inafanyika vizuri sana kwakweli. Mimi nimepita huko, kabla hata sijaja ofisini. Miradi mingi inafanyika vizuri sana. Kwahiyo niwapongeze, mnafanya kazi nzuri ya kusimamia na hata kubuni miradi. Mambo ni mazuri,” amesema Kapinga.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia) akimkaribisha Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dodoma, alipofika kuwatembelea na kuzungumza na Menejimenti, Novemba 7, 2023.

Pamoja na pongezi hizo, Naibu Waziri ameishauri REA kuendelea kuwajengea uwezo wasimamizi wa miradi, ili waweze kuifahamu na hivyo kuisimamia vizuri katika hatua zote tangu inavyoanza hadi inapokamilika kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nafahamu wengi ni wapya na wako baadhi ni wazuri na wengine siyo wazuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutoijua vizuri miradi, kutokuifuatilia vizuri au uzembe tu.

“Hivyo nashauri muwajengee uwezo na kuhakikisha wanasimamia miradi kuanzia mwanzo, kwani ndiyo muda sahihi na unaofaa,” amefafanua.

Akieleza zaidi, Kapinga amesema aina ya ufuatiliaji unaotakiwa katika miradi ni pamoja na kuhakikisha pesa zinazotolewa kwa Wakandarasi zinatumika kwa matumizi stahiki pamoja na kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa wakati.

Aidha, ameishauri REA kuhakikisha kuwa inajenga mazuri ya miradi inayotekelezwa ili inufaishe jamii kwa kipindi kirefu yaani vizazi na vizazi.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), baada ya kikao baina yao alipotembelea Ofisi za Wakala Novemba 7, 2023. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Athumani Mbuttuka na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy.

Akizungumzia suala la uunganishaji wateja katika maeneo ambayo miradi mbalimbali ya umeme imekamilika, Kapinga amesema ni vyema nguvu ya kutosha ikaelekezwa katika kuhakikisha wananchi wanaelimishwa na kuhamasishwa kuunganisha umeme ili miradi hiyo iwe na tija kwakuwa Serikali inatumia fedha nyingi sana kutekeleza miradi hiyo.

“Suala la kuunganisha wateja tulichukulie kwa uzito kama ambavyo tunaweka uzito mwingi katika utekelezaji wa miradi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema, Wakala unaahidi kuendelea kujituma pamoja na kuleta ubunifu katika kuharakisha upatikanaji wa nishati bora maeneo ya vijijini.

Aidha, ameongeza kusema kuwa Wakala ataendelea kupokea maelekezo na miongozo kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Nishati na Mamlaka nyingine za Serikali katika kutimiza wajibu wake na kufanikisha malengo na azma ya Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi waishio vijijini kupitia upatikanaji wa nishati bora katika maeneo yao.

Sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao, Novemba 7, 2023. Naibu Waziri alitembelea Makao Makuu ya Wakala hiyo jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.