Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
KANISA la Tanzania Assemblies of God (TAG) limepongezwa kwa kutoa huduma nzuri ya kiroho na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ili kusaidia jamii yenye uhitaji ikiwemo watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Deusdedit Katwale katika ibada maalumu ya Maadhimisho ya Miaka 85 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo nchini na miaka 54 ya kanisa la Kitete Christian Centre (KCC) la Mjini hapa.
Akitoa salamu za serikali kwa niaba yake, Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Rose Kilimba amepongeza kazi nzuri inayofanywa na kanisa hilo ya kuhubiri injili ikiwemo kuanzisha miradi ya kijamii kwa ajili ya wananchi.
Amebainisha kuwa kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhubiri injili iletayo amani, kuliombea taifa na kuanzisha miradi yenye maslahi kwa jamii.
‘Napenda kuwahakikishia kuwa Halmashauri ya Manispaa Tabora na Serikali kwa ujumla tunaunga mkono shughuli zenu zote, na tutaendelea kuwapa ushirikiano wakati wote ili kufanikisha shughuli zenu za kiroho na kimwili pia’, amesema.
Naibu Mstahiki Meya amewapongeza kwa kuanzisha Mradi wa Shule ya Komputa ili kutoa Mafunzo hayo kwa jamii na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Huduma ya Mtoto (compassion) kilichopo kanisani hapo.
Aidha amelipongeza kanisa la KCC kwa kuanzisha Mfuko wa kusaidia watoto wasio na uwezo ili kuwawezesha kupata elimu na mahitaji mengine ya msingi badala ya kutegemea wafadhili kutoka nje, hili ni jambo jema, endeleeni hivi hivi.
‘Mhesh. Mkuu wa Wilaya anawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya ya kusaidia waumini kiroho ikiwemo miradi yote inayoendelea kutekelezwa, ameahidi kuwachangia kiasi cha sh mil 1 katika shughuli zenu’, amesema.
Awali Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG Jimbo la Tabora ambaye ndiye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kitete Chrisrian Centre (KCC) Rev.Paul Meivukie amesema kuwa kanisa la TAG lilianzishwa rasmi mwaka 1939.
Amefafanua kuwa ibada hiyo ni maalumu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kanisa hilo kubwa hapa nchini kutimiza miaka 85 na kanisa la mahali pamoja la KCC kutimiza miaka 54 tangu lianzishwe katika Mkoa huo mwaka 1970.
Aidha amemshukuru Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini Dkt Barnabas Mtokambali kwa maono makubwa, uongozi mahiri, utulivu na uongozi bora ambao ndiyo umewezesha kanisa hilo kufika hapo lilipofika na kupata mafanikio makubwa.
Rev.Meivukie amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu na kutoa uhuru wa kuabudu kwa madhehebu yote, aliahidi kuwa wataendelea kumwombea ili taifa lizidi kustawi.
Ametaja miradi ya kijamii inayotekelezwa na kanisa la KCC na la Kitaifa kuwa ni mradi wa komputa, mradi wa kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, kituo cha maendeleo ya mtoto na kijana na ujenzi wa jengo jipya la kisasa la ibada.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto