Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa jitihada zake nzuri za kuendeleza utekelezaji mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere la kufua umeme ili kuongeza uzalishaji wa nishati hiyo hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Jimbo la Tabora Rev.Paul Meivukie ambaye pia ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG-Kitete Christian Centre la mjini hapa alipokuwa akitoa salamu za sikukuu ya Krismasi katika ibada iliyofanyika kanisani hapo.
Alisema hatua ya hivi karibuni ya Rais Samia kuzindua tukio la ujazaji maji katika Bwawa hilo lililopo Rufiji Mkoani Pwani ili kuwezesha Bwawa hilo kuanza kujaa maji ni hatua muhimu sana inayostahili kupongezwa.
Alibainisha kuwa mradi huo ambao ulianza kutekelezwa na Rais wa awamu ya 5 Hayati Dkt John Pombe Magufuli utakapokamilika utaleta faraja kubwa kwa watanzania kwani utaweza kuzalisha megawati 2,115 hivyo kumaliza kero ya kukatika katika nishati hiyo iliyopo kwa sasa.
‘Nachukua nafasi hii kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazofanya kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati ili kuongeza kiwango cha nishati ya umeme inayozalishwa hapa nchini’, alisema.
Aidha Rev. Meivukie alipongeza hatua ya serikali kuanza kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima na kutoa bei elekezi kwa wananchi, aliomba utaratibu wa uuzaji mbolea hiyo kuwekwa vizuri ili kuwaepushia wakulima usumbufu wanaopata.
Alisisitiza kuwa Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Mungu na kuendelea kumwomba ili amani na utulivu uliopo sasa uendelee kudumishwa na kumtaka kila mmoja kuchapa kazi kwa bidii.
Akinukuu maandiko matakatifu katika kitabu cha Wathesalonike wa 2 aya 3:10 alisema kila mtu anapaswa kufanya kazi na asiye fanyakazi asile, na kuongeza kuwa mvua zinazoendelea kunyesha sasa ni fursa muhimu sana ya kufanya kazi.
Alitoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuhimiza watoto wao kufanya kazi ili familia zao ziwe na chakula cha kutosha na sio kuacha watoto wao kupaka wanja tu. ‘Hakuna sababu ya watu kuteseka kwa njaa wakati mvua zipo’, aliongeza.
Rev. Meivukie aliwataka waumini wa kanisa hilo na madhehebu mengine ya dini kuendelea kumwomba Mungu ili mwaka 2022 umalizike kwa amani na utulivu na awape mwaka 2023 uliojaa neema na baraka na usio na majanga.
Aliongeza kuwa wakiendelea kumwomba Mungu atabadilisha majira mabaya kuwa neema na baraka na lolote lililo kinyume na mapenzi yake halitatokea kamwe katika taifa letu.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â