November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi wa mgodi Namtumbo kuanza

Na Netho Sichali, TimesMajira Online, Nyasa

KAMPUNI ya Uchimbaji madini ya Uranium Mantra inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi mdogo, Juni mwaka huu katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Mahusiano wa Kampuni ya Mantra Khadija Pallangyo wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi katika maadhimisho ya ya Siku ya Wafanyakazi Duniani,Mkoa wa Ruvuma yaliyofanyika Mbamba bay wilayani Nyasa.

Meneja wa Mahusiano ya jamii ya Kampuni ya Mantra Khadija Pallangyo Akiwa na mfanyakazi mwenzie akiwakilisha kampuni ya Mantra katika maadhimisho ya ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mkoa wa Ruvuma yaliyofanyika Mbamba bay Wilayani Nyasa hivi karibuni.

Pallangyo amefafanua kuwa kampuni hiyo inajishughulisha na kufanya utafiti wa madini ya Uranium katika Wilaya ya Namtumbo na mpaka sasa tayari wamekamilisha utafiti wa madini na wanatarajia kuanza ujenzi wa mgodi mdogo wa awali ifikapo Juni mwaka huu.

Aidha ameongeza kuwa kampuni hiyo imeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwani inathamini mchango unaofanywa na wafanyakazi wa kampuni ya Mantra pamoja na kushirikiana na wafanyakazi wengine duniani.

“Kampuni ya Mantra inajishughulisha na kufanya utafiti wa uchimbaji madini ya Uranium katika Wilaya ya Namtumbo na Tayari tumekamilisha utafiti na tunategemea kuzindua ujenzi wa mgodi mdogo wa awali, Juni, mwaka huu na tuko hapa kwa ajili ya kusheherekea sikukuu ya Wafanyakazi kwa kutambua mchango wa wafanyakazi wetu katika Kampuni ya Mantra na wadau wa maendeleo Mkoa wa Ruvuma.

“Hivyo tumeona tuhudhurie na tuwawakilishe wafanyakazi wetu ili tuongeze mshikamano na wafanyakazi wetu,’ amesema.