December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni ya JatuPLC yaitisha,mkutano Maalum wa dharura wa wanahisa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

 KAMPUNI ya Jenga Afya Tokomeza Umaskini (JATU) PLC imeitisha mkutano maalum na wadharura kwa lengo la kuwakutanisha wanahisa zaidi ya 10,000 wa kampuni hio ili waweze kuwapitisha wajumbe wa bodi ambao hatua za kuwapata zilishafanyika kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu JATU Plc, Mohamed Simbano amesema mkutano huo wa dharura wa JATU utafanyika kwa njia ya mtandao (zoom) kesho.

Amesema mkutano huo  unakuja wakati ambao kampuni hiyo inapitia changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha.”Watu watakaoudhuria kwenye mkutano huo ni wale wote wenye hisa katika kampuni hiyo kwa wanahisa ambao watashindwa kuhudhuria au kuteua mwakilishi watapaswa kutuma fomu za uwakilishi mapema kabla ya siku ya kesho,”amesema na kuongeza 

“Mbali na wanahisa hao kuhudhuria,kikao hicho kitapitisha wajumbe wa bodi ili kuruhusu wafanye kazi ya kuweza kuirudisha kampuni yetu kwenye uzalishaji,” amesema Simbano

Amesema wanafanya mkutano huo mara baada ya kumleta mtaalamu wa masuala ya biashara, fedha na utawala kutoka Uholanzi, Ben Philpsen aliyekuja kwa njia ya kujitolea ili kuisaidia kampuni hiyo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo madeni.

“Kila mwanahisa wakati wa kuingia katika mkutano huo utakaofanyika kwa njia ya mtandao yaani zoom lazima aandike jina lake sahihi kama linavyosomeka kwenye cheti chake hisa ili uongozi uweze kupitia na kuthibitisha kama kweli ni mwanahisa kinyume na hapo ataondolewa kwenye kikao.

“Nia yetu ni njema tunataka kila mtu aweze kushiriki kwakuwa hatutaki mwanahisa yeyote apoteze haki yake ya msingi ya kupiga kura kuchagua wajumbe pindi itakapofika,” amesema Simbano

Amesema mara baada ya mkutano huo kufanyika na kupata wajumbe wa bodi watakuwa na jukumu la kurudisha kampuni kwenye uzalishaji na ndani ya miezi mitatu wataitisha mkutano mkuu ambao utafanyika katika ukumbi mkubwa hivyo wanahisa wote watahudhuria na kutoa maoni yao.

“Baada ya mkutano wa kesho sasa bodi pamoja na viongozi watakuwa na jukumu la kurudisha JATU kwenye uzalishaji na ndani ya miezi mitatu wataitisha mkutano mkuu ambao utafanyika kwenye ukumbi mkubwa maana tutakuwa na uwezo wa kumudu gharama ndogo ndogo za kila siku katika endeshaji ambazo kwa sasa zimesimama.