Na Suleiman Abeid
Timesmajira Online, Shinyanga
KAMPUNI ya Brampem Global Investment Co. Ltd ya mkoani Shinyanga imeingia matatani baada ya kubainika kutengeneza barabara chini ya kiwango na kuchelewesha kukamilisha kazi aliyopewa nje ya muda wa mkataba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, mkandarasi huyo amebainika kuchelewesha kukamilisha mradi wenye mkataba namba AE/001/2022-2023/SHY/W/16 wa matengenezo ya mara kwa mara.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari mjini Shinyanga, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Mwamba Masanja amesema mradi huo unahusisha kazi kuu za uchongaji wa barabara, kuweka vifusi, kushindilia na kuchonga mitaro.
Amefafanua kwa kusema kazi hiyo ilitakiwa kukamilika Aprili 24 mwaka huu lakini haikukamilika kwa wakati mbali ya mkandarasi kuongezewa muda wa ziada wa siku 75 tangu Aprili 28 hadi Julai 12 mwaka huu sambamba kukatwa fedha ikiwa ni adhabu ya kuchelewesha mradi kwa mujibu wa mkataba.
“Baada ya kufanya ufuatiliaji tulibaini ucheleweshaji wa ukamilishaji wa mradi wa matengenezo ya mara kwa mara (Periodic Maintenance), matengenezo ya kawaida na uboreshaji wa vipande vya barabara katika barabara za kata ya Chamaguha, Ngokolo, Ndembezi, Kambarage na Mwasele,
“Kazi hii inatekelezwa chini ya usimamizi wa Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) wilaya ya Shinyanga kwa gharama ya shilingi 236,606,000.00 ukihusisha kazi za uchongaji wa barabara, kuweka vifusi, kushindilia na kuchonga mitaro ulitakiwa ikamilike Aprili mwaka huu lakini kazi haikukamilika,” ameeleza Masanja.
Masanja ameendelea kueleza kuwa mbali ya mkandarasi huyo kuongezewa muda hadi kufikia Julai 12, mwaka huu lakini hakuweza kukamilisha kazi hiyo na hivi sasa yupo kwenye kipindi cha makato ya fedha ikiwa ni adhabu ya kuchelewesha mradi kwa mujibu wa mkataba.
Mkuu huyo wa TAKUKURU amefafanua kuwa mbali ya ucheleweshaji wa mradi huo pia mkandarasi amebainika kuutekeleza chini ya kiwango kinyume na “standard specification of roads works 2000” ambayo ni sehemu ya mkataba wa kazi husika.
“Tulimshauri msimamizi wa mradi ambaye ni TARURA imtake mkandarasi arudie kazi zote alizotekeleza chini ya kiwango ili thamani ya fedha iweze kuonekana na ushauri huo umefanyiwa kazi na mpaka sasa marekebisho yenye thamani ya shilingi milioni 76 yameishafanyika,” ameeleza Masanja.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameipongeza TAKUKURU kwa hatua yake ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ambapo wameomba ufuatiliaji zaidi katika miradi yote ya umma ikiwemo ujenzi wa majengo ya Serikali.
“Binafsi nimefarijika kusikia taarifa hii ya TAKUKURU, ninawapongeza kwa kazi nzuri ya ufuatiliaji, niwaombe tu wasiishie kwenye miradi ya barabara lakini pia wafanye uchunguzi kwenye ujenzi wa majengo ya umma mfano Zahanati, Vituo vya afya na vyumba vya madarasa kwenye shule zetu,” ameeleza Abdalah Sube.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, Solomon Nalinga amesema iwapo TAKUKURU wataendeleza utaratibu huo wa ufuatiliaji ni wazi wakandarasi wengi wataacha udanganyifu katika utekelezaji wa miradi ya umma wanayopewa kuitekeleza.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba