December 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampuni ya Bima za Maisha ya Jubilee yashinda tuzo ya huduma bora

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni ya Jubilee Life Insurance  Corporation of Tanzania Limited imeibuka kidedea kati ya makampuni yote ya bima  baada ya kushinda tuzo ya utoaji bora wa huduma za Bima ya Maisha kwa wateja wake hivi karibuni.

Tuzo zilizotolewa na Chartered Institute of Customer Management zililenga kuangalia utoaji huduma wa makampuni mbalimbali kwa wateja wake zilifanyika Four Points by Sheraton jijini Dar Es Salaam ijumaa iliyopita, imepongeza na kutoa tuzo kwa Kampuni ya Jubilee Life Insurance ikiwa ni kampuni yenye kujali na kuzingatia ubora katika utoaji huduma kwa wateja wake kipengele cha bima.

Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bi. Helena Mzena alisema tuzo hiyo inaendelea kuwapa hamasa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuahidi kuendelea kuwahudumia wateja wao kwa viwango vikubwa.

“Tuzo hii ni heshima kubwa sana kwetu na inaendelea kutupa hamasa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi, mwaka jana 2023 ulikua ni mwaka wa mafanikio makubwa na sasa tumejipanga ipasavyo kuwahudumia wateja wetu kwa viwango vya juu kabisa, na tungependa kuwafahisha wateja wetu kuwa Jubilee Life Insurance imejikita katika kuwekeza kidigitali ili kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma kwa urahisi  ” alisema 

Pia Mzena aliwashukuru waandaaji wa tuzo hizo lakini pia wateja wao wote kwa kuendelea kuwaamini 

“Jubilee Life Insurance inawashukuru sana wateja wake na wale wote walioshiriki kwenye mchakato wa kupata mshindi wa tuzo ya huduma bora na inaendelea kutoa bima bora za Maisha zinazolinda ndoto za wateja wake na wapendwa wao”