Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
KAMPENI ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid Campaign inatarajiwa kuanza kutikisa mikoa 19 kuanzia mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha wanapata msaada wa kisheria.
Hayo yalitangazwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba, Mary Makondo, wakati akizungumza kwenye maonyesho ya biashara ya kimataifa yanayoendelea kwenye viwanja vya saba saba jijini Dar es Salaam.
Alisema kwenye mwaka wa fedha ulioisha walifanikiwa kuwafikia wananchi 500,000 na kwamba wameshapanga ratiba ya namna ya kuhakikisha wanaifikia mikoa yote iliyobaki.
“Tumeshapanga kila mwezi angalau tumalize mkoa mmoja kwa hiyo wananchi wawe na amani kwamba sisi tutawafikia kupitia kampeni hii mikoa yote ambayo hatujapita tutahakikisha tunapita mmoja baada ya mwingine,” alisema
Alisema kwenye kampeni hiyo wanashirikiana na wadau mbalimbali kama Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania Bar Association.
Alisema mbali na wadau hao, mpango huo unafanyakazi kwa karibu na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia.
“Kwenye kampeni hii tumepata ushirikiano mkubwa sana wa mahakama, Jeshi la Magereza nao wamekuwa wakiratibu vizuri namna ya sisi kuwafikia wafungwa na mahabusu na kuwapa msaada wa kisheria na wadau wengine tunaomba tuendelea kusaidiana kufanikisha jukumu hili zito la kusaidia wananchi,” alisema
Alisema pia wamekuwa wakifanyakazi kwa karibu na wasaidizi wa kisheria paralegals na aliwaomba kuendelea kushirikiana na serikali ili iwe rahisi kuwasogezea huduma za msaada wa sheria kwani wengi hawana uwezo wa kumudu kuweka mawakili kwenye mashauri yao.
Aliwataka wasaidizi wa sheria ambao wako kwenye mikoa mbalimbali nchini wajitoe kwa nguvu zao zote kuwasaidia wananchi kwa kuwaandalia nyaraka za kuwasilisha mahakamani na kuwashauri namna ya kupata haki zao.
“Pia wahakikishe wanawapatia usuluhishi wa migogoro yao kwasababu kuna aina ya migogoro ambayo mnaweza kukaa nao mkazungumza na mkafikia mwafaka hata bila ya kufikishana mahakamani,” alisema
Alisema huduma hiyo ni endelevu na wasaidizi wa kisheria watakuwa wanapita kwenye mikoa mbalimbali hata ile ambayo wamepita kuwapa elimu wananchi kuhusu masuala ya kisheria.
Mama Samia Legal Aid Campain ilizinduliwa Aprili mwaka jana kwa kuanzia mkoa wa Dodoma na mpaka sasa tayari mikoa saba imefikiwa.
Mbali na Dodoma mikoa mingine iliyofikiwa ni, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga na Njombe na Ruvuma.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango