Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas imezindua rasmi kampeni yake ya ‘Anzia Ulipo’ jijini Dodoma, ikilenga kuwahamasisha wakazi wa Kanda yake ya Kati, kuanza safari yao ya maendeleo kwa kutumia kile walicho nacho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kati, Said Idd amesema Kampeni hiyo inaakisi dhamira ya Yas, kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuwawezesha Watanzania kujikwamua kiuchumi na kijamii.
Kujikwamua huko kumejikita hasa katika maeneo yanayoendelea kukua kwa kasi kama Dodoma na mikoa ya Kanda ya Kati.

“Tunazindua kampeni hii tukiwahimiza Wakazi wa Kanda hii kutambua kuwa hakuna muda mwafaka zaidi ya sasa.
“Mafanikio hayaangalii ukamilifu bali hatua ya kwanza na ujasiri wa kuanza,” amesema Idd.
Amesema, kampeni ya Anzia Ulipo imelenga kuwapa Watanzania motisha ya kutumia teknolojia katika kuboresha maisha yao na kufikia malengo binafsi.
Aidha, amesema tayari Yas imewekeza kwenye mtandao wa kisasa wa intaneti ya kasi (4G na 5G) ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana hata maeneo ya pembezoni.
“Leo hii, mwalimu anaweza kufundisha darasa mtandaoni akiwa kijijini, mfugaji wa nyuki kufuatilia bei ya asali kwa kutumia simu, na kijana mbunifu hapa Dodoma kuonyesha kazi zake kwa dunia nzima. Haya yote yanawezekana kwa kutumia teknolojia,” ameeleza.

Katika hotuba yake, Idd pia amewashukuru wakazi wa Kanda ya Kati kwa kuzipokea chapa za Yas na Mixx kwa moyo mkunjufu, akibainisha kuwa mwitikio huo ni uthibitisho wa kiu ya wananchi kupata huduma bora, rahisi na zenye kuleta tija katika maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo amesisitiza kuwa, Yas itaendelea kuwasaidia vijana, wakulima, walimu na wajasiriamali kwa kuzindua huduma na kampeni zinazowawezesha kukuza maarifa, kupanua mitandao yao ya biashara, na kufikia malengo kupitia majukwaa ya kidijitali.
“Tunafahamu changamoto za ajira rasmi, ndiyo maana tunatambua na kuunga mkono nguvu ya vijana wanaoamua kujiajiri kupitia ujasiriamali.
“Yas tunawaambia, msisubiri hali iwe kamilifu, anzeni pale mlipo. Ndoto zenu ni halali, uwezo wenu hauna kikomo, na fursa zipo. Tunachohitaji ni uthubutu,” amesema kwa msisitizo.



More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani