December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamishna wa madini asisitiza umuhimu wa CSR kwa jamii zinazozunguka migodi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amebainisha kuwa, wajibu wa Kampuni za Madini katika jamii (CSR) unapaswa kutekelezwa na wamiliki wa migodi ili kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi.

Amesema hayo Novemba 21, 2022 katika kikao cha kupokea maoni ya wadau kuhusu wajibu wa kampuni za madini kwa jamii (CSR) katika ukumbi wa Halmashauri ya jiji Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

Dkt. Mwanga amesema CSR ni muhimu ikatolewa kwa jamii zinazozunguka migodi ili wananchi wanufaike na uwepo wa rasilimali madini.

“Hata kama CSR isingetajwa kwenye sheria bado nyinyi kama wamiliki wa migodi mngepaswa kuwajibika nalo kwa sababu linatengeneza mahusiano mazuri kati ya wamiliki wa migodi pamoja na wananchi wanaozunguka katika maeneo hayo,” ameongeza Dkt. Mwanga.

Ameeleza, kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini kinaeleza wazi kuwa mmiliki wa leseni ana jukumu la kuandaa mpango wa mwaka wa wajibu wa kampuni kwa jamii uliokubalika kwa pamoja na mamlaka ya Serikali ya Mtaa husika.

“Sheria inawataka kwenye Halmashauri waweze kuandaa miongozo ya namna ya kusimamia shughuli za CSR,” amesema.

Vile vile, ameeleza umuhimu wa wadau wa Sekta ya Madini kushirikishana kila wakati katika matukio mbalimbali hususan katika Rasimu ya Kanuni za CSR.

Kikao hicho cha siku moja kinahudhuriwa na wawakilishi wa mgodi wa Ruvuma Coal, STAMIGOLD, North Mara Williamson Diamond Limited, Shanta, Songwe, GGM, wadau wa Sekta ya Madini kutoka Geita Manispaa, Mara, Msalala, Shinyanga Mjini, Mbinga, Lindi, Songwe na taasisi za Kiraia ikiwemo HAKI RASILIMALI.