Na Mwandishi wetu, timesmajira
KAMISHNA wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda ameeleza kufurahishwa kwake na ubora wa viwango vya ujenzi wa karakana ya matengenezo ya magari na mitambo iliyojengwa Kanda ya Kati ya TAWA wilayani Manyoni, karakana inayotajwa kuwa ni kubwa kuliko karakana zote zilizojengwa na taasisi hiyo.
Ameyasema hayo Januari 14, 2024 akiwa katika ziara yake Makao Makuu ya Kanda ya Kati ya TAWA wilayani Manyoni, ziara yenye lengo la kukagua shughuli za uhifadhi na utalii zinazotekelezwa na TAWA wilayani humo.
“Nimetembelea na kukagua karakana, kimsingi nimeona imejengwa vizuri na pia nimeona ina uwekezaji mkubwa wa vifaa vitavyotumika na nina imani hii karakana itatusaidia sana” amesema
Akibainisha sababu za kuifanya karakana hiyo kuwa kubwa wilayani humo, Kamishna Mabula amesema Manyoni ni katikati ya nchi na ni sehemu inayofikika kwa urahisi, hivyo kutokana na ukubwa wake itatumika kutengeneza magari si tu ya Kanda ya Kati bali ya taasisi nzima.
Aidha, Kamishna Mabula ameuelekeza uongozi wa Kanda hiyo kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa karakana ikiwa ni pamoja na kuwapeleka wataalamu wa vifaa hivyo ili iweze kusimamiwa na kuendeshwa Kisasa.
Vilevile Kamishna Mabula ametumia ziara hiyo kuwahimiza Maafisa na Askari wote wa TAWA kurejea mpango mkakati wa taasisi hiyo ambao unafikia kikomo Mwaka 2026 ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amefafanua kuwa mpango mkakati wa TAWA una malengo makuu matatu ambayo ni kuhakikisha rasilimali ambayo TAWA imepewa kusimamia inakuwa salama, pia kuhakikisha wateja wote wa taasisi wakiwemo wawekezaji wanapata huduma na kuridhika na huduma inayotolewa na lengo la tatu ni kuhakikisha TAWA inafanya kazi kwa ufanisi na tija.
Kamishna huyo amesisitiza kuwa malengo hayo hayataweza kutimia bila kuishi katika tunu za taasisi hiyo ambazo ni uadilifu, kufanya kazi kwa ushirikiano, kutenda kazi kwa ubunifu pamoja na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Naye Kamishna Msaidizi Ulinzi wa Rasilimali za Wanyamapori,Hadija Malongo akimwakilisha Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TAWA kwa kuwezesha ujenzi wa karakana hiyo ambayo kukamilika kwake kutasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya magari ambayo ilikuwa changamoto kubwa
Mradi wa ujenzi wa karakana hiyo umegharimu zaidi ya TZS Million 217.
More Stories
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima
Dkt.Biteko aagiza Kituo cha huduma kwa wateja Tanesco kusukwa upya
Rais Samia aridhishwa na uongozi safi wa Mwinyi