January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamishna atakiwa kupanua wigo wa utalii nchini

Na Sophia Fundi, Timesmajira Online, Karatu

WAZIRI wa maliaasili na Utalii, Dkt Pindi Chana amemtaka Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro (NCAA), Dkt. Elirehema Doriye kupanua wigo wa utalii kwa kusimamia vivutio mbalimbali vilivyoko katika meneo yao.

Dkt. Pindi Chana ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Hafla ya kivishwa cheo na uapisho wa Kamishna wa Mamlaka hiyo iliyofanyika leo Desemba 23 katika viwanja vya ofisi za mamlaka.

Amemtaka kamishna kuhakikisha anasimamia vivutio vilivyoko na kuviboresha ikiwemo vivutio vya Olduvai, mapango ya Amboni, Magofu ya Engaruka na mengineyo.

Aidha, waziri ametoa maelekezo kwa Kamishna kuhakikisha anaboresha miundombinu ya barabara, madaraja na huduma za maji zinapatikana muda wote ili watalii wafurahie huduma zilizoko hasa kipindi hichi cha sikukuu.

Alimpongeza kwa kipindi alichokaa kabla ya kuapishwa kusimamia mapato ya Mamlaka ambapo kwa kipindi cha Julai hadi Novemba 2024, wamekusanya zaidi ya bilioni 138, huku watalii laki 551 wa nje na watalii laki 201 wa ndani wakitembelea vivutio vilivyoko katika hifadhi zetu.

“Nakupongeza kwa kipindi kifupi ulipoteuliwa na leo umeapishwa, tumeona juhudi zako na ufanisi katika kazi kwani mmekusanya kiasi hicho na watalii kuongezeka, naomba muongeze kasi zaidi katika majukumu yenu ya uhifadhi,” amesema Dkt. Chana.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Venance Mabeyo amesema kama bodi wako tayari kushirikiana katika uongozi wake kwa kusimamia mambo makuu matatu ambayo ni uhifadhi endelevu, kuendeleza utalii na maendeleo ya jamii.

Amesema, ishara ya kuaminiwa kuteuliwa kwako na Rais, si kwa Rais tu bali na wadau wa sekta ya uhifadhi hivyo uzoefu wako, uwezo wako, weledi wako, uzalendo wako na maono yako yanatarajiwa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kufikia malengo yake.

Akizungumza baada ya uapisho Kamishan Doriye amemshukuru Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa ya kumteua kuwa Kamishna wa mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, ambapo ameahidi kusimamia dhamana hiyo kubwa.

Ameahidi kusimamia maliasili kwa ajili ya kizazi hichi na kijacho na pia kusimamia uhifadhi endelevu na kukuza utalii wa kimkakati kwa kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma ndani ya hifadhi ili Ngorongoro ibaki kuwa kivutio kinachoongoza duniani.

Pia, amesema ataimarisha mahusiano mazuri baina ya jamii inayozunguka hifadhi na inayoishi ndani ya hifadhi na pia kukabiliano na changamoto zilizoko kwani changamoto ni sehemu ya safari.

Hata hivyo ameahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kusimamia maslahi yao kwa kupata mafunzo, motisha stahiki ili kuimarisha hali ya kazi.