Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.
UTOAJI wa elimu bure wa msaada wa kisheria wa Mama Samia kampeni umezinduliwa leo Januari 24,2025 mkoani Katavi huku wananchi wengi wakijitokeza kujengewa uwezo ili watambue haki zao na kujipigania.
Kampeni hiyo ni mpango wa serikali kuanzisha mkakati mpya wa kitaifa wa utoaji msaada wa kisheria na maeneo yanayopewa kipaumbele katika awamu hii ya miaka mitatu ni pamoja na masuala yahusuyo unyanyasaji wa kijinsia,migogoro ya ardhi na mirathi.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ameweka wazi huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi inasambazwa kuanzia maeneo ya mjini hadi vijijini ambako ndiko kiini cha mizozo ya ukosefu wa haki unaotokana na ufahamu duni wa kisheria.
Akiwa katika viwanja vya shule ya msingi Kashauriri manispaa ya Mpanda, Mrindoko ameeleza kampeni hiyo itasaidia kulinda na kutetea wananchi wanyonge kupata haki zao ambayo ni adhima ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
‘’Tunaamini kuzingatia sheria na utawala bora ni msingi wa maendeleo ya taifa letu na kupitia kampeni hii itasaidia sana wananchi wetu wa hali ya chini tupatiwa ufumbuzi wa matatizo yao yanayowasumbua kuhusiana na masuala ya kisheria kwani tutakuwa na wanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria,Wanasheria kutoka taasisi binafsi kwa kushirikia na wanasheria waliopo kwenye halmashauri na mkoa wetu wa katavi” amesema.
Kiongozi huyo, amefafanua kampeni hiyo inaaksi falsafa ya 4Rs ya Rais Dkt Samia kwa kujenga maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kuimarisha misingi utu itakayosaidia kupata ufumbuzi matatizo yanayowakabili wananchi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Franklin Rwezumla, amesema kampeni hiyo itaenda sanjali na utoaji elimu ya uraia kwa viongozi mbalimbali ikiwemo wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama za ngazi zote,watendaji wa kata katika mikoa yote nchini.
Ili kutimiza nia hiyo, Wizara imeanzisha madawati ya kisheria katika halmashauri zote nchini kwa kushirikiana na waratibu wa kisheria katika maeneo husika yataendelea kutoa huduma hata baada ya kumalizika kwa kampeni.
Kwa umuhimu huo, Wataalamu wa sheria wako tayari kufika katika shule za msingi na sekondari kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu ili waweze kufahamu wajibu wao kama wanafunzi na walimu wakiwa shule, majumbani na maeneo mengine na kuwa taa kwa jamii.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na sheria Boniface Butondo, amesema bunge mtawalia litaendelea kutoa fedha za kuwezesha kampeni hiyo ili iweze kufikia wananchi wengi nchini.
Butondo amesema kama wananchi wengi wanaoishi vijijini wenye matatizo ya kisheria katika ardhi, mirathi, ndoa na migogoro mingine wakifikiwa itawawezesha kuishi maisha yao kwa amani.
Magdalena Kishiwa, Mkazi wa mtaa wa Kawasejese manispaa ya Mpanda amempongeza Rais Dkt Samia kwa kuja na kampeni hiyo huku akisema “ Rais huyu hakika ni mama anayetambua sio maisha ya wananchi wake pekee bali anatambua matatizo yanayowakabili na kutafuta ufumbuzi wa haraka”
Mama huyo wa watoto wanne amefurahishwa baada ya kupata huduma ya vyeti vya kuzaliwa vya watoto wake wawili katika moja ya banda la utoaji huduma la RITA lililopo katika eneo la viwanja vya shule ya msingi Kashauriri ambapo kampeni hiyo ya siku kumi ya msaada wa kisheria ya mama Samia inatolewa.
More Stories
Serikali yaimarisha uchumi wa kidigitali kukuza biashara mitandaoni
RAS Tanga aipongeza Lushoto DC kuvuka lengo mapato ya ndani
Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu latakiwa kutoa huduma bora za kisheria