Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
KAMATI mpya ya ushauri wa kisekta ya chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) imetakiwa kutoa maoni na ushauri utakaowezesha kuboresha mitaala na uandaaji wa mitaala mipya itakayoendana na wakati, kutilia mkazo mahitaji ya soko, ujuzi na kuboresha usimamizi wa mafunzo kwa vitendo.
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akimwakilisha Waziri wa Elimu kuzindua Kamati hiyo pamoja na mafunzo ya uaandaji mitaala ambapo amesema kufanya hivyo kutasaidia Chuo kuendelea kutoa wahitimu bora na wenye ujuzi stahiki.
Prof. Mdoe pia ameitaka Kamati hiyo kuangalia mahitaji ya taaluma na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kushauri maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho ili kujumuisha maarifa ya kisasa, umahiri, kujenga ubunifu, kukuza stadi za kazi na viwango vya kimataifa.
“Nimefarijika kujulishwa kuwa wajumbe wateule wa Kamati wanatoka katika makampuni/Taasisi ambazo majukumu yake yanaendana na fani zinazofundishwa hapa MUHAS. Kwa msingi huo sina wasiwasi na weledi, ujuzi na uzoefu wenu. Ni matumani yangu kuwa ujuzi na uzoefu wenu mkubwa utakuwa na manufaa katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma hapa chuoni,” amesema Prof. Mdoe.
Ameongeza “kupitia Mradi wa HEET tumetenga Shilingi bilioni 18.23 ambazo zitatumika kuhuisha na kuandaa mitaala mipya zaidi ya 300 ya Taasisi za elimu ya juu lengo ni kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na kujibu mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi,”
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa HEET kwa MUHAS amesema utajikita katika kukarabati na kujenga Kampasi ya Mloganzila (Ndaki ya Tiba) na Kigoma, kuboresha miundombinu ya kujifunza na kufundishia, kuhuisha au kuandaa mitaala, kusomesha watumishi, kuweka miundombinu ya kisasa ya TEHAMA pamoja na kuweka mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kufundishia na utawala.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dkt. Harrison Mwakyembe amemuhakikishia Prof. Mdoe kuwa watasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa umakini ili uweze kuwa na matokeo chanya.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu ambae pia ni Mratibu wa Taifa wa Mradi wa HEET Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Kenneth Hossea amesema Mradi unaotekelezwa MUHAS ni kati ya miradi mitatu mikubwa katika Taasisi 23 zinazofaidika na mradi huu na kuwaomba ushirikiano ili kuhakikisha pamoja na kuwa mradi umechelewa kuanza utekelezaji wake uweze kufikia malengo.
Makamu Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Prof. Andrea Pembe amesema Chuo kinajivunia kuwa kitovu cha mafunzo katika nyanja ya afya na kwamba siku zote kitaimarisha ubora wa mafunzo yanayotolewa. Amesema pamoja na mafanikio yaliyoyapatikana ikiwemo ukuaji wa tafiti, Chuo kwa sasa kipo katika kuongeza nguzo kuu mbili ambazo ni kubadilisha ubunifu unaofanyika kuwa bidhaa ambayo itapelekea nguzo ya tano ambayo ni viwanda.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba