Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Daniel Sillo ( Mb) imefanya ukaguzi wa miradi mitatu (3) ya uboreshaji wa miundombinu ya kitalii iliyopo katika Pori la Akiba Mkungunero lililopo katika mikoa ya Dodoma na Manyara
Tukio hilo limehusisha ukaguzi wa miradi ya ujenzi ya barabara yenye kilometa 47.5, lango kuu la kuingilia wageni na eneo la kupumziki watalii “picnic site” yote ikigharimu kiasi cha shilingi Milioni 672.
Miradi hiyo imejengwa kwa kupitia fedha za Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya bajeti, Mhe. Daniel Sillo amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizi.
Aidha, Mhe. Sillo ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa usimamizi mzuri wa miradi hii na akasisitiza kuendelea kusimamia matumizi mazuri ya fedha za miradi ya maendeleo.
“Simamieni vizuri fedha za umma, ili zilete tija kwa kizazi cha sasa na baadae”.
Awali, Akizungumza wakati wa ukaribisho, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema uboreshaji wa miundombinu katika Pori la Akiba Mkungunero utatoa wigo mpana wa eneo hili kutembelewa na watalii kwa sababu ya miundombinu inayoendelea kuwekwa.
Kadhalika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka ameipongeza TAWA kwa nzuri na aliishukuru kamati kwa kutenga muda kwa ajili ya kupitia miradi hiyo.
Naye, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizi ambazo zimetolewa kwa kipindi muafaka wakati Taifa likijiandaa kupokea wageni wengi baada ya uzinduzi wa filamu maalumu ya “Royal Tour”.
Aidha ameishukuru kamati na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa.
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba