January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Bunge yampongeza Samia utekelezaji miradi NHC

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, amepongeza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa utekelezaji wa miradi mitatu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na ameagiza ikamilike kwa wakati.

Miradi hiyo mitatu ni pamoja na Samia Housing Scheme (SHS) uliyopo Kawe na mingine miwili ambayo ni Kawe711 uliyopo Kawe na Morocco Square yote ikiwa jijini Dar es Salaam.

Pongezi hizo zimetolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mzava, mara baada ya kutembelea miradi hyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua miradi hiyo, Mzava, amesema NHC kwa sasa hawana kisingizo tena cha kutokamilisha miradi hiyo, kwani tayari fedha zimeshatolewa.

“Kama kamati hatutamani kuona miradi hii inasimama au kwenda kwa kusuasua kwa sababu kisingizio kilikuwa ni fedha, lakini tayari Rais Samia ameshatoa fedha, hivyo tunawaomba NHC wawasimamie wakandarasi wakamilishe miradi hii mikubwa kwa wakati,” alisema.

Aidha, Mzava ambaye ni Mbunge wa Korogwe Vijijini amesema kuwa
kamati hiyo imebaini kuwa kazi hiyo isingefanyika vizuri kama siyo nia, moyo, mtazamo na maono ya Rais Samia kutoa kibali kwa NHC kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

“Tunampongeza Rais kwa kazi hiyo nzuri ya kuruhusu NHC kupata fedha ili kuendelea na miradi, pia tunaipongeza NHC kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hii,” amesema

Amesema kamati imefurahi na kuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi hiyo mitatu kwani kati ya miradi hiyo mmoja ni wa muhimu unakwenda kuacha alama ya Rais Samia.

Hata hivyo, alisema kuwa miradi miwili ambayo ni Morocco Square na Kawe 711 ilisimama kwa muda mrefu kutokana na maelekezo ya Serikali ya kulitaka shirika hilo liweze kufanyakazi vizuri hasa katika kutafuta fedha za kutekeleza miradi.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda alisema wanamshukuru Rais Samia kwa kuridhia miradi hiyo kuendelea kwa kuwa hapo awali ilisimama kwa muda kupisha mambo ya kiserikali.

Amesema mradi wa Morocco Square umeshakamilika kwa asilimia 99 na tayari majengo yaliyopo hapo yameshachukuliwa na wapangaji na wanunuzi kwa asilimia 90 na hiyo ni ishara kwamba miradi sasa inafanya vizuri.

“Tutaendelea kusimamia maelekezo ya Rais Samia kuhakikisha kwamba miradi hii inamalizika kwa wakati na inaleta tija kwa wananchi na nchi kwa unumla,” alisema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah alisema shirika linaendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati na chini kupitia mradi wa huo SHS ambapo utekelezaji wake unaendelea.

Amesema mradi huu wa SHS ni mradi wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi mazuri anayofanya Rais Samia ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora nchini.

Amesema asilimia 50 ya nyumba hizo zitajengwa katika mkoa wa Dar es Salaam ,asilimia 20 mkoa wa Dodoma na 30 mikoa mingine.

“Mradi huu wa SHS utakuwa na nyumba 5,000 ambapo utatekelezwa kwa awamu na utagharimu kiasi cha sh.bilioni 466,”alisema.

Nyumba 560 zinaendelea kujengwa na hadi kufikia Juni 30,2024 ujenzi wa nyumba hizo umefikia asilimia 65.

Mradi huu wa Kawe utagharimu sh.bilioni48.27 na hadi sasa takribani kiasi cha sh.biliioni 21.88 zimeshatumika.,” amesema

Amesema mauzo ya mradi huo yamefikia asilimia 100 na tayari NHC imepokea malipo ya awali ya kiasi cha sh.bilioni 31.2 na kiasi kilichobaki ni sh.Bilioni 45.5 zinaendelea kukusanywa.

Akizungumzia mradi wa Morocco Square amesema umekamilika kwa asilimia 99 na shughuli za upangishaji tayari umeanza kwa baadhi ya maeneo ikiwemo hoteli yenye vyumba 81.

Aidha amesema jengo lenye nyumba za makazi 100,tayari nyumba 71 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobaki yanaendelea.

Amesema hadi sasa katika nyumba za makazi na biashara zilizouzwa shirika limekusanya kiasi cha sh.bilioni 30 na kiasi cha sh.bilioni 35.9 kinaendelea kukusanywa huku eneo la maduka limeshapangishwa kwa asilimia 98 na kwa sasa upangaji wa bidhaa unaendelea ili kufungua maduka hayo mwezi julai mwaka huu.

Akizungumza mradi wa Kawe 711, amesema mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 40 ambapo una nyumba 422, pamoja na sehemu za biashara ambao ulianza Novemba 2014 na ulisimama 2018.