Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAJUMBE wa Kamati ya Bunge ya Bajeti wameshauri wananchi waendelee kupewa elimu kuhusu uhakiki wa stempu za kielektroniki kwenye bidhaa wanazonunua.
Hayo yalisemwa jana kwenye semina ya kamati hiyo na kampuni ya Societe Industrielle de Produits Alimentaire (SICPA) ya nchini Uswisi ambayo imeingia ubia na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
SICPA ina zaidi ya miaka miwili nchini ikiwa imetoa ajira kwa Watanzania 171 na ina mfanyakazi mmoja wa kigeni ambaye ndiye meneja mkuu akifanya idadi ya wafankazi wote kuwa 172.
Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Hasna Mwilima akichangia mada iliyowasilishwa na Meneja Mkuu wa SICPA kwa upande wa Tanzania, Xavier Davard, alisema kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi wa vijijini ili wajue namna ya kubaini bidhaa feki.
Davard alitoa mada kwa kamati hiyo kuelezea namna mfumo wa stempu za kielektroniki (ETS) unavyofanya kazi na ulivyosaidia kuokoa upotevu wa mapato ya Serikali, ufanyaji wa biashara haramu na namna ya kubaini bidhaa feki.
Mfumo huo kwa sasa umeanza kwenye bidhaa za pombe, hatua ya pili ni vinywaji baridi kama maji na soda. Kwa sasa bado wanafanya utafiti kwenye viwanda vya bidhaa za mafuta na sementi.
Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge mbali na kuupongeza mfumo huo kwa kusaidia kudhibiti mapato ya nchi, alihoji kwa nini nchi za jirani kama Kenya na Uganda hazitumii mfumo huo na badala yake mfano uliotolewa hapo ni wa mataifa ya nje ya Afrika.
Davard alisema nchi jirani na Tanzania ziko kwenye mchakato wa kutumia mfumo huo, ambapo kwa Kenya wataanza na bidhaa za pipi na chokleti.
Alisema matumizi ya stempu za kielektroniki za kodi kwa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa yalianzishwa kuchukua nafasi ya matumizi stempu za karatasi ambazo matumizi yake yalihusishwa na vitendo vya ukwepaji kodi pamoja na bidhaa bandia kwa kiasi kikubwa.
Davard alisema wanufaika wa mfumo huu ni Serikali, wazalishaji, waagizaji na watumiaji ambapo faida zake ni kulinda mapato ya Serikali kwa kuzuia bidhaa bandia.
Pia, mfumo huo unamuwezesha mtumiaji kutambua bidhaa yenye stempu halali kwa kutumia simu ya mkononi, kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa kutengeneza wigo sawa wa ushindani kwa wafanyabiashara wote wanaozalisha na kuingiza bidhaa nchini.
Davard katika mada yake alisema pia, mfumo huo unawezesha ufuatiliaji wa bidhaa kutoka viwandani, mipakani, bohari zilizoruhusiwa, majengo ya kutunzia bidhaa, sokoni hadi kwa mlaji.
Alisema pia, unawezesha usimamizi wa bidhaa zinazotengenezwa au zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
Kuhusu mafunzo ya namna ya kutumia mfumo kwenye simu ili kubaini bidhaa feki, Davard alisema wametoa mafunzo kwa wafanyakazi wa TRA na kuwapa kifaa kidogo cha kutambua stempu feki.
Alisema mafunzo mengine ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TRA yamesimama kutokana na ugonjwa wa corona, lakini yataendelea hali itakapokuwa nzuri.
Davard alisema mbali na wafanyakazi wa TRA, pia wateja wanaweza kutumia simu zao kwa kupakua programu ya TRA kitakacho mwezesha mteja kubaini bidhaa feki.
Davard alisema hata kwa simu za ‘kitochi’ mteja anaweza kubaini bidhaa feki kwa kutuma namba iliyopo kwenye stempu na itampa majibu kama ni halali au ni feki.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam