October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Amani Rukwa yaandaa siku ya kuliombea Taifa kuwa na uchaguzi wa amani

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Rukwa

KATIKA kuhakikisha Uchaguzi Mkuu nchini unafanyika kwa utulivu na amani, Kamati ya Amani mkoani Rukwa imeandaa siku maalum kwa ajili ya kuliombea taifa kufanikisha uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28,mwaka huu.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Rukwa Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la KKKT (kulia) akijadiliana na Kaimu Katibu wa Kamati hiyo Mchungaji Emanuel Sikawe (katikati) pamoja na Mjumbe wa Kamati hiyo Sheikh Hassan Said Hassan wa Baraza la Shia Mkoani Rukwa

Akitoa tamko hilo kwa niaba ya kamati,Kaimu Katibu Mtendaji wa kamati hiyo Mchungaji Emanuel Adam Sikazwe wa Kanisa la Monravian alisema kuwa amani ni tunu pekee ambayo Watanzania wamepewa na Mungu na hivyo wana kila sababu ya kuiheshimu, kuilinda na kuitunza ili isitoweke wala kuvunjika.

Aidha, aliwataka vijana kujiepusha na vishawishi vya maandamano, pamoja na kutumika kuanzisha fujo kwani kwa kufanya hivyo mkono wa sheria utawakabili na kutahadharisha kuwa endapo vurugu hizo zikitokea watakaoathirika ni wale wasio na nguvu na wasiojiweza.

“Sisi viongozi wa dini kama wadau wa amani tumekubaliana kuwa na siku maalum ya kufanya maombi Oktoba 26 na maombi haya pamoja na dua vitafanyika kwenye viwanja vya Sekondari ya Kizwite kuanzia saa tatu asubuhi, hivyo tunawasihi raia wa dini zote kuhudhuria siku hiyo ili kuungana pamoja kumuomba Mungu kuwaleta viongozi waliochaguliwa na kutuondolea ghasia na fujo zitakazoweza kujitokeza siku hiyo ya uchaguzi.

Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki kwenye kikao cha Kamati ya Amani ya Mkoa wa Rukwa.

“Upande wa viongozi wa dini, imebainika kuna watu wanaojitokeza wakiungana na watu wanaohamasisha vijana kufanya fujo ili waweze kuandamana kipindi cha uchaguzi, sisi kama viongozi wa Kamati ya Amani ya Mkoa, tunawaomba viongozi wote wa kidini wasijihusishe kabisa na siasa katika kuelekea uchaguzi mkuu.” alisisitiza

Hayo yamejiri baada ya wajumbe wa kamati hiyo kukutana na kutoa tamko la pamoja kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa pamoja na wadau wote wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi kuzingatia misingi ya sheria na kuheshimu taratibu zilizowekwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Askofu Ambele Mwaipopo wa kanisa la KKKT alisisitiza kuwa kamati inatoa tamko hilo kwa nia njema hasa kwa kujali amani nchini tunu ambayo nchi imepewa na Mwenyezi Mungu na wana wajibu wa kuiendeleza wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ili shughuli za wananchi ziendelee kwa usalama