December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu RC amaliza mgogoro wa wafanyabiashara Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Rashid Chuachua ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kaliua amefanikiwa kumaliza mgomo wa wafanyabiashara wa halmashauri ya manispaa Tabora uliopelekea kufungwa maduka kwa masaa 12.

Akizungumza na umati wa wakazi wa manispaa hiyo wakiwemo wafanyabiashara katika eneo la soko kuu mjini hapa jana Kaimu RC alisema mgomo huo umeathiri wananchi kwa kiasi kikubwa kwa kukosa mahitaji yao tangu asubuhi hadi jioni.

Alieleza chanzo cha mgomo kuwa ni Watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani hapa kuvamia na kuvunja stoo ya mfanyabiashara Celestine Livasi usiku Juni 30, bila ya mhusika kuwepo na kuchukua mzigo wa vitenge vipatavyo 638.

Alisema kitendo hicho kililalamikiwa na wafanyabiashara hao wakidai ni cha uonevu na kutofuatwa taratibu jambo lililopelekea kugoma kufungua maduka kwa siku nzima huku viongozi wao wakiwasilisha malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa.

Kaimu RC alibainisha kuwa miongoni mwa madai ya wafanyabiashara hao ni kurudishwa kwa mzigo uliochukuliwa na Maafisa wa TRA na kuongeza kuwa kama mzigo ulikuwa na tatizo taratibu zilipaswa kufuatwa na sio kuvamia na kupora kwa nguvu tena usiku.

Baada ya kukutana na wawakilishi wa wafanyabiashara hao na Maafisa wa TRA akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kusikiliza kilio cha wafanyabiashara wote, alihitimisha kwa kutoa maelekezo yaliyoafikiwa na wafanyabiashara hao hivyo kusitisha mgogo huo.

Miongoni mwa maelekezo aliyotoa ni Maafisa wa TRA kuondoa mara moja kufuli waliloweka kwenye mlango wa stoo hiyo, halmashauri ya manispaa hiyo iweke utaratibu wa ukusanyaji ushuru na tozo mbalimbali na kuwataka kuondoa tozo zinazoumiza wananchi.

Aliongeza kuwa mzigo ulioleta sintofahamu amearifiwa kuwa umetoka nje ya nchi na ulikuwa unafuatiliwa na Maafisa wa Forodha kutoka Makao Makuu ukidaiwa kusafirishwa kinyemela pasipo kulipiwa ushuru.

Hivyo akaeleza kuwa wamekubaliana mnunuzi (Celestine) awasilishe risiti za manunuzi ya mzigo huo kwa Meneja wa TRA ili kujiridhisha kama umenunuliwa kihalali, kama zipo apewe mzigo wake na kama hazipo taratibu zifuatwe.

Aidha Kaimu RC alipiga marufuku watendaji wa mitaa, vijiji na kata kufunga biashara za wananchi kwa kisingizio cha kutofanya usafi au kutolipa ushuru, na kushauri wapewe elimu kwanza badala ya kutumia nguvu kubwa.

Alipotafutwa na gazeti hili mfanyabiashara Celestine alieleza kuwa mzigo huo ameununua kihalali jijini Dar es salaam na nyaraka zote anazo na kuahidi kuziwasilisha kwa Meneja wa TRA Mkoa kama alivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa.

Umati wa wafanyabiashara wa halmashauri ya manispaa Tabora wakimsikiliza Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Dkt Rashid Chuachua ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kaliua, alipokuwa akiongea nao kuhusiana na mgogo wao uliopelekea kufungwa maduka kwa masaa 12 jana. Picha na Allan Vicent.