January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kafulila akuna kichwa kuokoa tril. 1/- Dar

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KAMISHNA wa Idara ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha, David Kafulila, amenza kukuna kichwa kuona namna ya kuokoa sh. Bilioni 4 zinazopotea kwa siku jijini Dar es Salaam sawa na sh. trilioni 1 kwa mwaka kutokana na msongamano wa foleni za magari.

Kafulila, ametoa takwimu hizo za upotevu wa kiasi hicho cha fedha, mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika kikao cha kukisikiliza mawasilisho zaidi ya manne ya wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Kafulila, upotevu huo wa fedha unatokana na hesabu ya muda ambao wananchi wanaotumia kukaa barabarani kwa sababu ya foleni, hali inayopunguza muda wa kazi.

Aidha, foleni hizo zimekuwa zikichangia upotevu wa mafuta ya kwenye vyombo vya moto kutokana na kukaa barabarani kwa muda mrefu, ikilinganishwa na kama kusingekuwa na foleni.

Amesema Jiji la Dar es Salaam kwa wingi wake wa watu na maeneo yake, halipaswi kuwa na foleni ya kiasi hicho, lakini changamoto ya miundombinu ndiyo inachangia msongamano.

Hivyo, amesema wanatakiwa kukabiliana na changamoto ya miundombinu, ambapo zipo njia tatu za kumaliza tatizo hilo.

Ametaja njia hizo kwa ni pamoja na reli za mjini, barabara za kutoa watu katikati ya jiji pamoja na barabara za za mabasi ya mwendokasi.

“Ili kukabiliana na foleni kuna uimarishaji wa kwanza ni kualika wawekezaji kwa ajili ya kuwezesha reli ya mjini, ambayo siyo nzito kama ya SGR na tofauti ya gharama na barabara siyo kubwa sana, pili Tanroads kujenga barabara za kutoa watu katikati Jiji ili kupunguza msongamano na tatu ni DART ambapo tuna awamu sita, tunatafuta wawekezaji katika awamu zote wakipatikana

sasa hivi katika maeneo yote maana yake tutarahisisha usafiri, hizo zote ni jitihada za kuhakikisha zinatoa watu katikati ya jiji na kupunguza msongamano”amesema Kafulila.

Pia, amesema kwa kufanya hivyo maana yake kwenye uchumi wataokoa zaidi ya sh. bilioni 4 kwa siku ambazo zinapotea kutokana na msongamano kwa mujibu wa tafiti.

“Hivyo tunavyosema kwamba tunataka wajenge uchumi kwa kutumia mitaji binafsi tafsiri yake ni kuipa Serikali nafasi ya kuwekeza kwenye maeneo mengine,” amesema Kafulila.

Amesema ni kazi ya Serikali kujenga reli, barabara za Dar es Salaam na kila kitu, lakini ukivuta mitaji ya binafsi ikifanya hiyo, hivyo Serikali itatumia fedha hizo katika maeneo ambayo hayawezi kuvutia mitaji.

Ametolea mfano kwamba Serikali ina uhitaji mkubwa wa kuwekeza kwenye elimu ili kupata rasilimali watu wenye ubora, kwani duniani ya leo haishindani kwa kiasi cha dhahabu, eneo la kilimo, idadi ya vituo vya utalii, bali kwa ubora wa watu wanaotenda kazi.

“Dunia leo tunashindana kwa ubora wa binadamu, tafiti zinaonesha kwenye mataifa makubwa 13 kiuchumi asilimia 62 ya utajiri wao unatokana na rasilimali watu, ubora wa binadamu maana yake nini?

Ni watu wenye maarifa na afya,mtu bora dunia anachangia asilimia hiyo katika uchumi wa nchi tajiri, wakati ufanisi wa taasisi unachangia uchumi kwa asilimia 25 kwenye hizo nchi,”amesema Kafulila na kuongeza;

“Ufanisi wa taasisi maana yake hivi nyie mnachukua muda gani kushughulikia jambo fulani, uamuzi ambao unachukua miaka saba kufanya wenzio wanachukua wiki moja siku saba kushughulikia, rasilimali za nchi zinachangia asilimia ndogo na siyo kwamba hazina utajiri mkubwa, ila zina vitu vingi vya kuonesha.”

Amesema ili kujenga watu wenye ubora, lazima Serikali iweke fedha nyingi kwenye elimu na afya na mambo ambayo yatamtengeneza huyo mtoto, lazima apate walimu bora na wakutosha,vitabu vya kutosha kumtengeneza awe bora kweli.

“Fedha nyingi zitapatikanaje, lazima Serikali ipunguze kufanya matumizi kwenye maeneo ambayo sekta binafsi inaweza ikafanya ili kusudi fedha hizo zielekekezwe kwenye maeneo ambayo sekta binafsi haiwezi kufanya.

Sekta binafsi haiwezi kumpa mtoto wako elimu bure. Na iwe na ubora itahitajika ulipe. Kama tunataka inabidi Serikali iwe na fedha nyingi za kuweka huko, itawekaje huko na ijenge barabara na reli za Dar es Salaam na uwekezaji mwingine?

Tunataka mitaji ya sekta binafsi ije isaidie kufanya maeneo mengi ili Serikali ifanye kwenye kujenga ubora wa binadamu, leo Tanzania kwenye ripoti ya ubora wa binadamu anafikia asilimia 40 ya kile alichopaswa kuwa nacho na ili afikie asilimia 80 lazima ajengewe mazingira bora zaidi na afya bora,”.