Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
UONGOZI wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake Kiuchumi Kata ya Kimara na viongozi wa majukwaa yote ya Kata hiyo, wamefanya ziara katika shule ya Sekondari Kimara Kutwa, iliyopo kata ya Kimara wilaya ya Ubungo.
Ziara hiyo waliambatana na Diwani wa Kata Arch. Ismail Mvungi, Afisa Mendeleo wa Kata hiyo na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilungule A, Kaini Asalile.
Katika ziara hiyo iliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, kumetolewa elimu ya ukatili wa kijinsia na upendo kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Pia, wanafunzi hao walipatiwa zawadi kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu kwa kila kidato, wanafunzi sita wenye nidhamu shuleni hapo sambamba na ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike.
Zawadi hizo hazikuishia upande wa wanafunzi tu, bali na kwa walimu wa shule hiyo.
Mwalimu Mkuu alipatiwa zawadi ya usimamizi bora, Mwalimu wa Nidhamu alipatiwa zawadi ya uongozi bora upande wa nidhamu, mwalimu anayeongoza kwa somo lake kufanya vizuri kwa ufaula upande wa mchepuko wa sayansi pamoja na biashara.
Diwani wa Kata ya Kimara, Ismal Mvungi, aliahidi kuanza kuwafundisha somo la Hisabati Jumatatu, wiki ijayo kwa kujitolea kama alivyowahi kufanya hivyo mwaka uliopita. Pia aliwataka wanafunzi kuacha tamaa na kuzingatia masomo.
Kwa upande wake Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kata ya Kimara, Saida Bawazir, ametoa ombi kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo kuandaa siku na muda mahsusi kwa ajili ya kuwapatia wanafunzi hao elimu juu ya maadili, makuzi na ukatili wa kijinsia.
Amesema, jukumu hilo litasimamiwa na uongozi wa jukwaa, ambapo Mwalimu mkuu amelipokea ushauri huo na kuahidi kulifanyia Kazi jambo hilo.
Pia, amesema ni vyema iandaliwe mikakati kwa kushirikiana uongozi wa Jukwaa na ofisi ya Diwani Mvungi ya kuwaangalia walimu wanaojitolea kufundisha shuleni hapo ili kupata moyo ikiwa ni kwa ajili ya kuwaongezea ufanisi.
More Stories
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi
SACP Katabazi: Elimu ya usafirishaji wa kemikali bado ni muhimu kwa watanzania