November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jokate: Rais Samia kielelezo cha uongozi imara wa mwanamke

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dae

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT, Jokate Mwegelo amesesema tayari wanawake wa Tanzania wameshapata kielelezo cha uongozi imara wa mwanamke kupitia Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo hakuna sababu ya kubaki nyuma na badala yake wengi waonyeshe uwezo wao kwa vitendo.

“Ni lazima tugombee ili tuongeze viongozi wanawake kwenye mitaa na vijiji, kwa sasa hatujafika hata asilimia 10, UWT tutakwenda kuhakikisha tunaongeza ushiriki wa wanawake.

“Ifike mwisho wanawake kuwa wasindikizaji na kuwapigia kura wanaume, wakati hata sisi tuna uwezo wa kugombea na kushika nafasi mbalimbali, UWT itahakikisha kama kuna mwanamke anagombea atapitishwa na chama na atakwenda kushinda,” alisema Jokate.

Jokate ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari uliohusisha pia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa UWT mkoa wa Dar es Salaam.

Jokate amesema umoja huo utawapigania wanawake watakaojitokeza kushiriki uchaguzi huo, kwani idadi ya wanawake wanaoongoza mitaa na vijiji haizidi asilimia 10, hivyo kuna kila sababu ya namba hiyo kuongezeka kupitia uchaguzi huo.

Amewataka wanawake kuwaunga mkono wenzao watakaojitokeza kuwania nafasi hizo, kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa maendeleo kupatikana kupitia viongozi wanawake.

“Akijitokeza mwenzetu anagombea tusimkatishe tamaa, tumtie moyo kwa kumpigia kura, ili washinde kwa kishindo.Imezoeleka wanawake hatupendani, hatuwezi kuheshimiana kila mmoja na nafasi yake hilo limefutika chini ya uongozi wa Rais Samia,” amesema.

Jokate alizindua wimbo maalumu ulioimbwa na kundi la wasanii wa kike nchini ambao umebeba hamasa kwa wanawake na kuwakumbusha nafasi yao katika kujenga uchumi na ustawi wa Taifa.