March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasheria Mkuu :Mawakili wa Serikali kuweni na tabia ya kufanya kazi kwa haraka

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza  Johari amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuwa na tabia ya kufanya kazi kwa haraka, wakati na kwa kuzingatia ubora katika utoaji wa huduma za kisheria.

Johari aliyasema hayo leo wakati akizungumza na Mawakili wa Serikali kwenye Mafunzo maalumu kwa Mawakili  yanayofanyika Jijini Arusha ,alisema ni vema mawakili wa Serikali kufanya kazi kwa haraka na kwa wakati ili waweze kuiishi kauli mbiu ya weledi, ubora pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi. 

Amesema  kuwa mafunzo hayo kwa mawakili wa Serikali yatasaidia kuongeza umahiri kwa Mawakili wa Serikali na kuwawezesha kutoa huduma bora za kisheria zitakazochangia katika kuletea maendeleo kwa Taifa.

“Ili tuifikie Kaulimbiu yetu ya weledi na ubora ni lazima tuwe na tabia ya kufanya kazi kwa haraka na kwa wakati.

“Ili kuweza kutoa huduma bora za kisheria, kitu cha kwanza kwa Mwanasheria ni kuhakikisha kila jambo analifanya kwa wakati na kuzingatia ubora,”amesema Johari 

Awali akitoa mada kwa Mawakili wa Serikali Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole amewakumbusha Mawakili wa Serikali juu ya masuala muhimu ya kuzingatia wakati wanapoishauri Serikali ikiwemo kufahamu muundo na nyaraka mbalimbali za Serikali zitakazowasaidia kuelewa kwa kina majukumu na shughuli za Serikali. 

“Ili uwe Mwanasheria na mshauri mahiri ni lazima uyafahamu vizuri majukumu ya Serikali na pia kuhakikisha mnazisoma   na kuzielewa Sheria zinazosimamia Sekta mbalimbali ili waweze kuwa na wigo mpana wa utoaji wa ushauri kwa Serikali. 

“Kama Mwanasheria unatakiwa ufahamu mfumo wa kisheria wa sekta mbalimbali ili uweze kuwa mbobevu katika masuala ya kuishauri Serikali,”amesisitiza Njole 

Naye Jaji Mstaafu Sirilius Matupa akichangia mada amewasisitiza Mawakili hao  kuhusu weledi katika uandishi na uwasilishaji wa ushauri wa kisheria kwa wadau, ambapo amewasisitiza Mawakili hao kuwa mahiri katika nyanja mbalimbali za kisheria ili waweze kutoa ushauri utakaotatua changamoto zinazoweza kujitokeza.

“Mawakili wanatakiwa kutoa ushauri kwa kufuata misingi ya kisheria na kuwasilisha ushauri wao kwa weledi ili ushauri wanaoutoa uweze kuwa na tija na kutatua changamoto husika,”amesema  Jaji Matupa

Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali yameandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanafanyika Jijini Arusha kwa siku 5 ambapo yameanza  machi 24 na yataendelea hadi machi  28,2025 jijini Arusha.