January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JKT laing’arisha Msomera kwa kujenga nyumba bora,miundombinu ya barabara

Na Joyce Kasiki,Handeni

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la uzalishaji Mali (SUMAJKT) limekamilisha ujenzi wa nyumba 1000 katika awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 5000 kwa ajili ya wananchi wanaohama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha  na kuhamia katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga huku nyumba nyingine zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujenzi huo,Mkuu wa Tawi la Utawala JKT ambaye pia ni Kamanda Kikosi Kazi cha ujenzi wa nyumba hizo,Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema katika awamu ya kwanza JKT ilipewa kazi ya kujenga nyumba 402 ambazo tayari zilishakamilika na watanzania waliokubali kuhama kwa hiari kutoka hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera tayari walishahamia.

Amesema katika awamu ya pili wanayoendelea mayo inayohusisha ujenzi wa nyumba hizo 5000 ,nyumba 2500 zinajengwa katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni ,nyumba 1000 zinajengwa katika kijiji cha Saunyi mkoani Tanga na nyumba 1500 zinajengwa katika kijiji cha Kitwai B wilaya Simanjiri milani Manyara.

Brigedia Jenerali Mabena amesema,baada ya kupewa kazi hiyo JKT lilijipanga kuhakikisha linafanya kazi hiyo kwa weledi na ubora unaokubalika na kujenga kwa wakati ili kutoa nafasi kwa wananchi wanachama kwa hiari kutoka Ngorongoro kuendelea kwenda kwenye maeneo hayo zinajengwa nyumba hizo.

“Baada ya kupewa jukumu hili JKT lilitafuta namna ya ujenzi wa nyumba hizo na ikaona namna bora ambayo inaweza kwenda na wakati lakini pia kutumia gharama nafuu na kuwa na nyumba bora ,tukaona iwe ni katika mpango wa operesheni ambapo Maafisa na Askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania ,watumishi wa Umma na Vijana wa JKT washiriki katika ujenzi huo.”amesema Brigedia Jenerali Mabena na kuongeza kuwa

“Lakini pia pamoja na kutumia rasilimali watu ,vifaa ,mitambo,magari ambayo yanamilikiwa na SUMAJKT pamoja na vikosi vya JKT viliratibiwa vyema na kupeleka eneo la ujenzi lengo kubwa lilikuwa ni kurahisisha kazi hiyo.”

Vile vile amesema katika kuhakikisha nyumba hizo zinajengwa kwa gharama nafuu,pia vifaa vilivyotumika kama vije matofari ,milango pamoja na madirisha vilizalishwa na JKT ambapo vikosi vyote vya JKT vimehusishwa katika kazi hiyo.

Wananchi wapongeza maendeleo Msomera

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wananchi wamepongeza Juhudi kubwa za kupeleka maendeleo zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan huku wakiwasihi wananchi ambao bado wapo Ngorongoro wafanye maamuzi sahihi ya kukubali na kuhamia kwa hiari yao kwenda Msomera na maeneo mengine yanayoandaliwa na Serikali kwa ajili yao.

Mwalimu Mkuu wa shule ya mfano wa mpango wa mtaala mpya yenye darasa la awali mpaka kidato cha nne Ibrahim Mhina amesema,shule hiyo ambayo 

imependekezwa kuitwa jina la Dkt.Isdory Philip Mpango imejengwa kwa ajili ya kupika wanafunzi wanaotoka Ngorongoro lakini kuandikisha wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza wenye umri wa kwenda shule.

“Tayari tumeshaanza kupokea wanafunzi wapya na mwitikio ni mzuri .”amesema Mhina 

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkababu kijiji cha Msomera Martine Singoya amempongeza Rais Samia kwa maendeleo makubwa yalipo Msomera hivi sasa yakihusisha bimba bora zinazojengwa na JKT.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mkababu kijiji cha Msomera Martine Singoya akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la shule ya mfano kwa mpango wa mtaala mpya iliyojengwa katika kijiji cha Msomera kwa ajili ya kupokea wanafunzi ambao wanahamia kwa hiyari kijijini hapo kutoka Ngorongoro.

“Mimi ni mzaliwa wa eneo hili,kabla ya uhamisho wa wananchi wa Ngorongoro kuja Msomera tulikuwa tunapata   shida ,tuliishi katika mazingira magumu ,wakati huo ng’ombe walikuwa wanatafuta maji mbali zaidi ya kilomita 18 lakini sasa hivi tunashukuru sana mradi huu wa mama Samia umeleta maendeleo Msomera,

“Kama hivi mnavyoona shule nzuri ya mfano imejengwa,sidhani kama kuna sehemu imejengwa shule nzuri kama hii ,huduma ya maji tunayo,barabara nyingi zimechongwa ,nakwambia Luna wenzetu ambao wanaenda Dar es salaam wakija huwa wanapotea,ni kwa sababu kuna muingiliano mkubwa wa barabara nyingi na kukifanya kijiji cha Msomera kuwa kama mjini.”amesema Singoya