Na Mwandishi wetu Timesmajira online
KATIKA kuadhimisha siku ya Moyo Dunia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kufanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo bure kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam na mikoa ya jirani.
Maadhimisho hayo ambayo kufanyika kila mwaka Septemba 29 yataenda sambamba na kambi hiyo ambayo itaanza kufanyika Septemba 28 na 29 katika kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe Jengo la Mkapa Health Plaza.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam mapema leo Septemba 27, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge amesema kambi hiyo itaanza saa mbili kamili asubuh hadi saa 10 jioni na itakuwa na madaktari Bingwa wa moyo pamoja na wataalamu wa lishe.
Amesema wataalamu hao wa lishe watatoa elimu ya lishe bora itakayowapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora ili kuepukana na magonjwa yasiyoyakuambukiza yakiwemo moyo ambayo yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
“Pamoja na upimaji huu kutakuwa na matembezi ya hiyari kesho Septemba 28, 2024 yatakayoanzia katika viwanja vya Jengo la Palm Village kuanzia saa 12 asubuh na kumaliza katika kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Kawe”amesema Dkt Kisenge
Dkt Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo amesema matembezi hayo ni kwa ajili ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi ya kujikinga na magonjwa yasiyoyakuambukiza yakiwemo Magonjwa ya moyo.
Aidha amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika matembezi hayo sambamba na kupima afya zao ili waweze kujua kama wanamatatizo ya Moyo ili waweze kuanza matibabu mapema kama wakigundulika kuwa wagonjwa.
Naye Daktari Mbobezi wa magonjwa ya Moyo,ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Hospital ya Dar Group (JKCI) Dkt Tulizo Shemu amesema viwango vya wagonjwa wanaotibiwa katika tawi hilo kwa siku inafikia wagonjwa 500 hadi 600.
Amesema wagonjwa hao wengi wamekuwa na matatizo ya moyo, huku wengi wao wakiwa ni watoto na watu wazima.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam