December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jinsi Sheria ya Usalama Barabarani ilivyokuwa mwiba kwa usalama wa watoto

Jinsi Sheria ya Usalama Barabarani ilivyokuwa mwiba kwa usalama wa watoto

Na Penina Malundo

SHERIA ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 imeelezea masuala ya kitaifa yanayohusu haki na ulinzi wa mtoto, ni sheria iliyochukua mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa yanayohusu haki za mtoto.

Na sheria hii inaweka bayana muundo unaolenga kumpa mtoto kinga pamoja na viwango kwa ajili ya utoaji haki kwa watoto kwa kuimarisha haki ya ulinzi, matunzo na haki za watoto Tanzania Bara.

Suala la usalama barabarani ni eneo mojawapo la kupewa ulinzi kwa mtoto kama sheria hiyo inavyosisitiza ulinzi kwa mtoto katika hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa.

Miongoni mwa eneo la kupewa ulinzi mtoto ndani ya gari ni pamoja na sehemu anayokaa mtoto ndani ya gari kuhakikisha anakuwa salama muda wote hususani gari linapotembea.

Vizuizi vya watoto ndani ya gari ni aina ya viti vyenye mikanda mahususi vinavyomlinda mtoto dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo ajali au breki za ghafla.

Vizuizi hivyo vinatengenezwa kulingana na umri, uzito,urefu na umri wa mtoto ambaye atatumia kiti hicho kukalia ndani ya gari na kumuweka salama pindi gari linapotembea.

Licha ya umuhimu wa vizuizi hivyo,Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 haijaweka wazi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kumlinda mtoto dhidi ya hatari yoyote inayoweza kutokea kwenye gari.

Mnamo Mei, 2011 katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulitangaza muongozo wa hatua kwa usalama barabarani 2011- 2020 ili kukabiliana na ongezeko la kasi kwa majeraha yanayohusiana na ajali za barabarani na vifo vinavyotokea ulimwenguni kote.

Miongoni mwa maazimio waliyopitisha ni pamoja na maeneo matano ambayo yatasimamiwa ikiwemo udhibiti ubora wa matumizi ya barabarani, ubora na uchakavu wa magari, utamaduni wa watumiaji wa barabara,kutoa elimu ya matumizi ya barabara pamoja na takwimu za ajali na vyanzo vya ajali.

Baraza hilo pia lilitoa mapendekezo ya kuendelea kusisitiza usalama wa barabarani katika mpango wa maendeleo endelevu hadi ifikapo mwaka 2030 katika lengo namba nne la kuhakikisha usalama wa barabarani unatekelezwa na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji uliopangwa katika Mpango wa Maendeleo Endelevu.

Mwaka 2017 Tanzania iliridhia mpango huo ambao unatarajia kuisha mwaka 2030, hivyo katika kuridhia huko nchi inapaswa kuendelea kutilia mkazo katika kuhakikisha sheria ya usalama wa barabarani inabadilishwa katika suala zima la vizuizi vya watoto wachanga kwa lengo la kuwaweka watoto katika sehemu salama pindi wanapotumia vyombo vya moto.

Katika kutekeleza Mpango wa Dira ya Maendeleo Tanzania (Vision 2025),Tanzania inapaswa kuona kuna umuhimu wa kubadilisha sheria ya mwaka 1973 ambayo ipo butu katika kuongelea masuala ya vizuizi vya watoto.

Hata hivyo, Ripoti ya mwaka 2018 ya Shirika la Afya Duniani (WHO),inaonesha kuwa nchi 84 tu ndizo zimeridhia sheria ya kulinda watoto wadogo kutokana na majanga ya ajali za barabarani na huku nchi 33 zenye idadi ya watu milioni 652, ndizo zina sheria za usalama barabarani za kulinda usalama wa watoto wadogo ambazo zinatambuliwa na WHO.

Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki, sio wanachama wa kundi hilo, tatizo kubwa zaidi ni kutokana na nchi za Afrika Mashariki (EAC) kutokuwa na sheria inayozungumzia matumizi ya vizuizi vya watoto katika magari.

Kwa mujibu wa tathimini ya WHO ya mwaka 2018, Sheria za usalama wa barabarani kwa watoto zikizingatiwa kikamilifu, zitapunguza ajali na vifo kwa watoto wadogo kwa asilimia 60.

WHO imekuwa ikieleza kuwa, watoto wachanga hadi wenye miaka 11, wanapaswa kutengewa kiti maalum kinachoweza kumtosha kulingana na uzito, umbo, urefu na hata umri.

Pia, vizuizi vya watoto ni viti maalum vyenye mikanda mahususi kumlinda pindi awapo katika gari kutopata mitikisiko au kutoka nje ya gari pindi ikitokea limepata ajali.

Licha ya umuhimu wa kuwa na viti maalum vya watoto kwenye magari, pia Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 haijaweka wazi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kumlinda mtoto dhidi ya hatari yoyote
inayoweza kutokea kwenye gari.

Mbaya zaidi katika Sheria hii ya Usalama Barabarani (1973), kifungu cha 39(4)(b) kinatambua watoto wawili, wenye umri unaozidi miaka mitatu na usiozidi miaka 12 kama abiria mmoja wanapopanda katika mabasi hali inayowafanya watoto hawa kukosa usalama pindi ajali inapotokea au dereva akifunga breaki ghafla.

Tumekuwa tukiona mikanda ya watu wazima tu katika magari mbalimbali huku vizuizi vya watoto kutoonekana kutokana na sheria kutowabana wamiliki wa magari na madereva.

Mara nyingi, ajali inapotokea usababisha watoto kupoteza maisha kutokana na wazazi kuwabeba au kuwapakata pindi gari linapotembea na wazazi kugeuza mikono kuwa vizuizi.

Akizungumza gazeti hili mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani ambae pia ni Mrakibu wa Kikosi hicho,Kamanda Deus Sokoni anasema, kundi la watoto wadogo ni miongoni mwa kundi maalum linalohitaji ulinzi wa ziada na kuangaliwa kwa ukaribu wanapokuwa barabarani.

Anasema, kundi la hilo la watoto wadogo ni kubwa ambalo linahitaji kuwa na uhitaji wa uangalizi wa maalum na jicho la pekee kuhakikisha kundi hili linakuwa salama muda wote.

“Umoja wa Mataifa pamoja na mikataba mbalimbali linaiangalia hili kundi, kwani lipo hatarini zaidi kuliko kundi la watu wazima linahitaji kinga ya pekee,’anasema na kuongeza

‘’Kinga ya pekee kwa watoto hao ni uangalizi wa ziada hasa watumiapo barabara kupitia azimio la umoja wa mataifa kila nchi mwanachama wa umoja wa mataifa anatakiwa kuhakikisha anakuwa na sheria ya usalama barabarani ambazo zinaangalia kwa upekee na umuhimu maisha ya kundi la watoto wadogo,’’anasema Afande Sokoni.

Aidha, anasema Tanzania hakuna sheria inayowalinda watoto wadogo moja kwa moja, kwani sheria iliyopo haijatamka mtoto mdogo alindwe vipi.

Afande Sokoni anasema, kwa kupitia maelezo ya Umoja wa Mataifa,Tanzania kama moja ya nchi wanachama ipo katika hatua mbalimbali ya kufanya marekebisho ya sheria ili sasa mtoto alindwe anapotumia barabara.

“Sheria ya Mwaka 1973 haijaweka wazi ni namna gani mtoto atalindwa, hivyo kama nchi kuna umuhimu wa kuifanyia marekebisho sheria hii na kuona ni namna gani mtoto mdogo atakavyotambulika katika ulinzi wake ndani ya gari,’’anasema na kuongeza

‘’Marekebisho ya sheria hiyo yanalenga ya kuwafikisha watoto wadogo kuwafikisha kwenye vizuizi ambavyo vitasaidia kupunguza kuondosha madhara kwa mtoto anapotumia usafiri wa barabara,’’anasema.

Anasema, kutokana na uhitaji wa kuwa na vizuizi vya watoto katika usafiri, takwimu za ajali za barabarani zinaonyesha uhalisia na uhitaji kuwa na vizuizi vya watoto kulinda maisha yao zinaonyesha kuwa mwaka 2017,watoto wa umri kati ya miaka saba hadi 12 jumla ya watoto 60 walifariki dunia na waliojeruhi wakiwa 230,huku kwa mtoto wa mwaka mmoja hadi miaka saba takwimu inaonyesha kuwa jumla ya watoto 11 walifariki dunia na waliojeruhiwa wakiwa 143 huku watoto wenye umri kati ya miaka 13 hadi 18 waliofariki walikuwa watoto 223,hii imefanya kuwe na jumla ya watoto 294 waliofariki na waliojeruhiwa ni takribani watoto 832 kwa mwaka huo.

Aidha, Kamanda Sokoni anasema katika kipindi cha mwaka 2018 watoto wadogo kati ya umri wa mwaka mmoja hadi saba jumla ya watoto wanne walikufa huku kwa umri wa miaka saba hadi 12 waliokufa walikuwa tatu walifariki na watoto kati ya umri wa miaka 13 hadi 18 takribani watoto 73 na kufanya jumla ya watoto 94 kufariki na waliojeruhi kuwa 258.

“ Kwa mwaka 2019,takwimu inaonyesha inaonyesha watoto wa umri kati ya mwaka mmoja hadi saba hakukuwepo na kifo,watoto kati ya umri wa miaka saba hadi 12 walifariki watoto 10 huku watoto kati ya umri wa miaka 13 hadi 18 takribani watoto 42 walifariki dunia na kufanya jumla ya watoto waliofariki kwa mwaka huo kuwa 52 na kujeruhiwa watoto 177,’’anasema.

Afande Sokoni anasema kasi iliyochangia kushuka kwa vifo kwa upande wa watoto ni utoaji wa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya moto wakiwemo madereva kwani kundi la mtoto mdogo ni kundi linalohitaji usimamizi.

Naye Ofisa Programu Masuala ya Usalama Barabarani kutoka Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS),Mercy Kessy anasema, sheria ya sasa ya usalama barabarani ya mwaka 1973 haiongelei kabisa masuala ya viti vya watoto ikiwa na maana kwamba hakuna kifungu chochote kinachoongelea utumiaji wa viti vya watoto kwenye magari.

Anasema, kutokana na sheria ya sasa ipo kimya,wadau wa masuala ya usalama barabarani ikiwemo TLS,wameweza kutoa mapendekezo yao ya kuwepo kwa mabadiliko ya sheria ya usalama wa barabarani kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani na vifo vitokanavyo na ajali.

Messi anasema, mojawapo ya mapendekezo waliyoyatoa ni pamoja na kuwepo na viti vya watoto katika magari binafsi pamoja na magari ya abiria ili kuokoa maisha ya watoto pindi ajali inapotokea.

“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watoto wanapokaa katika viti maalum kwenye magari yaani ‘child restraints’ kwa kuzingatia uzito na umri inapunguza kwa kiasi kikubwa ongezeko la vifo vya ajali kwa watoto,”anasema.

Anasema, kupitia mapendekezo ya wadau baada ya kufanya tafiti kwa nchi nyingine ni kuwa sheria ya sasa inayoenda kufanyiwa marekebisho iweke kifungu hicho cha kuweka ulazima wa magari binafsi na magari ya wa abiria kuweka vizuizi vya watoto katika magari yao.

Anasema, kwa tafiti zilizofanywa na Global Road Safety Partnership:Seat Belts Facts Sheets,2015inaonyesha nchi zinazotumia vizuizi vya watoto inapunguza madhara ya kupata ajali takribani asilimia 70.

Kwa upande wake mmoja wa waathirika aliyewahi kupata ajali akiwa na mtoto mdogo,Anna Yonah anasema kiti cha mtoto ni muhimu ndani ya gari pindi gari linapokuwa barabarani linatembea.

Anasema, kiti hicho kinakuwa msaada kwa mtoto pale breki ya ghafla inapofungwa na kuweza kumzuia asichomoke kutoka ndani ya gari na kutoka nje.

“Nakumbuka niliwahi kupata ajali nikiwa na mwanangu ila hatukuumia sana maana nilijifunga mkanda na mwanangu akiwa katika kizuizi chake,tulikuwa tukitokea nyumbani na kwenda matembezini.

‘’Mikanda na vizuizi ni muhimu sana ndani ya gari uokoa maisha ya watu pindi ajali inapotokea,’’anasema.