Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
MABADILIKO ya mfumo wa uondoaji yaka katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya umelipa ushindi wa nafasi ya pili katika mashindano ya usafi wa mazingira na afya ulioshindanisha majiji sita(6) yaliyopo Tanzania na kutunukiwa cheti pamoja na Sh.Mil.2
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 13 ,2024 Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mhe.Dormohamed Issa amesema ushindi huo umetokana na umoja ambao wananchi wa Jiji la Mbeya wameuonesha katika suala zima la kupambana na uchafu uliokuwepo siku za nyuma.
Aidha Issa amesema kuwa kwenye mashindano hayo yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya yalilenga usafi wa mazingira katika maeneo ya mikusanyiko ikiwemo Sokoni,vyoo vya umma,mitaro ya maji,maeneo yenye matumizi ya maji salama na matumizi ya vyoo vya kisasa.
Mshindi wa kwanza katika mashindano ni Jiji la Tanga lililopata jumla ya alama 124 kwa 124 huku mshindi wa pili Halmashauri ya jiji la Mbeya likiibuka na alama 97 kati ya 124 kwenye mashindano hayo ambayo yalizinduliwa na Makamu wa Rais Mhe.Philip Isdor Mpango Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani na vyeti kutolewa na Waziri mwenye dhamana ya afya Ummy Mwalimu.
Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Neemia Mwakatobe amesema awali kulikuwa na changamoto ya uwezo mdogo wa kumudu mfumo wa uondoaji taka kwa kutumia makontena 115 hali iliyosababisha kushika nafasi ya mwisho kwa miaka mitatu mfululizo katika mashindano hayo ya majiji sita ambayo ni Dodoma, Mwanza, Arusha, Dar es Salaam, Tanga na Mbeya.
Mwakatobe ameongeza kuwa baada ya mafunzo waliyoyapata Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro mwaka 2022, mfumo wa kutumia magari ya kuondoa taka ulianza na wazabuni wadogowadogo na kisha kuingia mkataba na shirika la Uchumi na Maendelo la jeshi la kujenga Taifa (SUMAJKT)sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kutumia mfumo huo uliowezesha kupata ushindi wa pili.
Mwakatobe kuwa kwasasa kilichobakia ni kuendelea kuielimisha jamii ya wananchi wa Jiji la Mbeya ili kuimarisha suala la tabia ya kutotupa taka ovyo.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu