October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jiji la Dodoma lapongezwa kwa ubunifu

Na Dennis Gondwe,TimesMajira Online,Dodoma

MENEJIMENTI ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa ubunifu wake kwa kutoka ofisini na kuwafuata wateja wa viwanja katika maeneo yao ya kazi kuwasogezea huduma hiyo na kuwaepusha na vishoka.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Mwantumu Salim alipokuwa akizungumza na timu ya kimkakati ya masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipomtembelea ofisini kwake kumshawishi kununua kiwanja Dodoma jana.

Salim amesema kuwa, zoezi la kuwafuata wanunuzi wa viwanja katika maeneo yao ya kazi ni hatua nzuri na jambo jema.

“Kwenye kutoa huduma, ukiweza kumfikia mteja wako ni faraja sana kwake. Nasema ni faraja kwa mteja kwa sababu kwanza unakuwa umemlinda dhidi ya vishoka, lakini pia unakuwa umemsaidia kuokoa muda ambao angeacha kutekeleza majukumu yake na kufuata huduma kwako.Baada ya nyie kuja ofisini kwangu nina hakika kiwanja nitapata. Na kama mngekuwa mnatufuata siku zote tungekuwa tumeshanunua viwanja siku nyingi,”amesema Salim.

Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa taasisi za serikali kubadilisha mtazamo katika utoaji huduma na kuwa kibiashara. “Umefika wakati sasa kwa taasisi za serikali tubadilike katika utoaji huduma na tuwe ‘business oriented’, kama Halmashauri tunatakiwa kuuza viwanja, tuuze viwanja ili kukusanya fedha kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii. Nina hakika hamtajutia muda huu mlioutumia, nina hakika mtarudi tena kwa huduma hii,”amesema Salim.

Awali Afisa Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Nuru Mariki amesema kuwa halmashauri hiyo imepima viwanja vya matumizi mbalimbali kwa ajili ya wananchi na wawekezaji.

“Halmashauri ya Jiji imepima viwanja vya makazi, makazi na biashara na huduma za viwanda katika maeneo mbalimbali. Viwanja hivyo vipo halmashauri vinauzwa na hakuna urasimu wa aina yoyote,”amesema.

Aidha, ameongeza kuwa halmashauri hiyo imetenga eneo maalum kwa ajili ya huduma ya viwanda katika Kata ya Nala.”Ni Nala Industrial hub’ ikiwa ni muitikio wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. ohn Magufuli inayosisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda,”alisema Maliki.

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweka kambi ya wiki nzima jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwasogezea huduma ya viwanja wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam.