Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam.
KAMISHNA wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu, CP. Suzan Kaganda Mei 13, 2024, Jijini Dar es Salaam, amefungua mafunzo ya siku mbili ya namna ya uwasilishaji wa nyaraka za mafao kupitia mfumo wa TEHAMA kwa Maafisa Wanadhimu Makao Makuu, Mikoa na Vikosi pamoja na Wasimamizi na Watendaji wa dawati la mafao wa Jeshi la Polisi.
Akifungua Mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, CP. Kaganda amewataka washiriki wa mafunzo hayo kusikiliza mada zote na kujifunza kwa umakini ikiwepo ya mfumo huo mpya wa uwasilishaji wa nyaraka za maombi ya mafao mbalimbali ya watumishi katika mfuko wa hifadhi ya jamii wa PSSSF.
Mfumo huo utasaidia uharaka wa kuwasilisha nyaraka za mafao na nyaraka hizo kufika kwa wakati katika mfuko wa PSSSF “mfumo huu utamrahisishia mwanachama kufuatilia yeye mwenyewe kujua kila hatua ya madai ya mafao kwa kupitia simu janja” Alisema CP. Kaganda
Pia mfumo huo utasaidia kuondoa kupotea kwa nyaraka za mafao wakati wa usafirishwaji “pia utasidia kujua eneo lenye mkwamo katika uwajibikaji wa kushughulikia ulipaji wa malipo ya mafao mbalimbali ya watumishi” aliongezea CP. Kaganda.
Vilevile CP. Kadanga amewakumbusha watendaji wa Jeshi la Polisi kujikita katika matumizi ya TEHAMA ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Polisi uliofanyika Septemba 4, 2023 Oyterbay, Dar es Salaam kwani suala la TEHAMA ndio lilibeba ujumbe wa kaulimbiu ya mkutano huo.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya jamii wa PSSSF Abdul-razaq Badru amesema wanaendelea kuboresha huduma za kimfuko ikiwa ni pamoja na maboresho ya kupunguza udanganyifu.
Katika hili alisema, “Tumeanzisha huduma mbalimbali,moja wapo ni PSSSF Kiganjani ili kuondoa usumbufu wa kupata taarifa za michango ya kila mwezi kwa wanachama wetu zoezi linalokwenda sambamba na kutoa elimu kwa wanachama na wadau wote wa PSSSF.
Vilivile Afisa Mkuu wa Rasilimali watu wa Benki ya NMB, Bwana Emmanuel Akunai amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuratibu na kusimamia mafunzo hayo yenye lengo la kuboresha ufanisi na huduma kwa watumishi wa Jeshi la Polisi.
Sambamba na hilo Bwana Akunai amesema Benki ya NMB itendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwezesha na kutoa udhamini katika matukio mbalimbali ya Jeshi la Polisi ili kuboresha utendaji kazi wa Jeshi hilo.
Aidha mafunzo hayo yamehitimishwa leo Mei 14, 2024 yakishirikisha Maafisa wanadhimu wa Kamisheni, Mikoa na Vikosi, sambamba na wasimamizi na watendaji wa madawati ya mafao ndani ya Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma,Tanzania Bara na Zanzibar.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi