December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jeshi la Polisi laweka wazi mikakati yake kuelekea uchaguzi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

JESHI la Polisi Nchini lisema kuelekea uchaguzi wa serikali za mtaa limejipanga kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika amani na utulivu.

Hayo yamesemwa jijini hapa Machi 28,2024 na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi David Misime wakati akiwasilisha mada kuhusu usalama wa wananchi wakiwemo waandishi wa habari katika kuelekea kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,mdahalo uliondaliwa na Muunganiko wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC).

Misime amesema wao kama jeshi la polisi moja ya majukumu yake ni kuangalia hali ya usalama na pamoja na kuhakikisha usalama unakuwepo eneo la uchaguzi.

“Tutahakikisha tunalinda vifaa vya uchaguzi,pia tutatoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya uchaguzi lakini tutazuia vitendo vya uvunjifu wa amani tutahakikisha watu wanakuwa salama wakiwemo waandishi wa habari,”amesema Misime.

Alitaja mikakati mingine kuwa ni kujenga mahusiano mazuri kati ya jeshi la polisi na wananchi kwa ujumla na kuendelea kusimamia sheria zinazotakiwa.

“Mimi nataka nikiwa na raia mwenzangu nataka tuzungumze kama binadamu wamoja tunaofanyakazi tofauti na siyo maadui,”amesema Misime.

Kwa upande wake Rais wa UTPC, Deogratius Nsonkolo aliishukuru serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mazingira sahihi na bora kwa waandishi wa Habari kufanya kazi.

Ametaja lengo la kuandaa mdahalo huo ni kushirikiana na wadau kuona ni namna gani ya kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wa Habari hususan katika kipindi kuelekea uchaguzi.

“Tunaipongeza serikali ya Awamu ya sita kwa kuboresha mazingira safi kwa waandishi wa Habari kwani sasa hivi waandishi wanafanya kazi kwa utulivu na katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu tunaamini mazingira yatakuwa bora Zaidi,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Dkt.Rose Reuben amesema katika kuelekea uchaguzi wandishi wa Habari wanatakiwa kuzingatia maadili.

“Wandishi wa habari zingatieni sana maadili hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi hakikisha taarifa unayotoa umejiridhisha na imetoka katika vyanzo vinavyotambulika ili kuondoa utata ambao unaweza kutokea baada ya kutoa taarifa za uongo,”amesisitiza.

Naye Ofisa Programu kutoka shirika la International Media Support (IMS) ambao ndio wafadhili wa mradi huo wa kutetea ulizi na usalama kwa waandishi nchini, Fausta Msokwa amesema lengo kuu la mdahalo huu ni kushirikiana na wadau mbalimbali na kuona ni namna gani tunaweza kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari hususani mwaka huu wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Amesisitiza kuwa dhamira yetu ya pamoja ni kuimarisha gurudumu la upatakinaji wa habari na uhuru wa kujieleza”.

Mdahalo huo ni wa pili Kitaifa ambapo wa kwanza ulifanyika Septemba 19, 2023 mwaka jana na umehudhuriwa na wadau mbalimbali pamoja na UTPC, Jeshi la polisi Tanzania, Viongozi wa dini, TAMWA, MISATAN, OJADACT, MCT, IMS, JOWUTA.

Kauli mbiu ya mdahalo huu ni “kutetea usalama wa mwandishi wa habari ni kutetea haki ya jamii kupata taarifa.”