December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jeshi la Polisi latoa Tahadhari

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama hususani katika kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka kwa kuwataka wananchi kutoa taarifa mbalimbali za viashiria au dalili za kihalifu ili wahusika washughulikiwe mapema kabla matukio ya kihalifu hayajatokea.

Ameyasema hayo Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro J. Muliro na kubainisha kuwa jeshi lina mipango mizuri ya mifumo ya kiusalama na kuwaomba wananchi waendelee kutoa taarifa mbalimbali za viashiria au dalili za kihalifu ili wahusika washughulikiwe mapema kwa mujibu wa sheria kabla matukio ya kihalifu hayajatokea.

TAHADHARI ZA KIUSALAMA KUELEKEA MCHEZO WA SOKA KATI YA SIMBA Vs AL AHLY NA YANGA Vs MAMELODI SUNDOWNS

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linafuatilia kuwa Ijumaa 29 Machi 2024 na Jumamosi 30 Machi 2024 majira ya saa 3 usiku kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam kutakuwa na michezo ya soka ya ligi ya mabigwa Afrika kati ya timu ya SIMBA ya Tanzania na AL AHLY ya MISRI utakaochezwa kuanzia saa 3:00 usiku. Na tarehe 30 Machi 2024 mchezo kati ya timu ya YANGA ya Tanzania na MAMELODI SUNDOWNS ya Afrika Kusini.

Kuelekea michezo hiyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo. Usalama siku ya mchezo utakuwa wa kiwango cha juu, maeneo yanayozunguka uwanja ndani, nje na barabara za kuingia na kutoka uwanjani. Ukaguzi utakuwa wa hali ya juu kabla ya kuingia uwanjani. Hairuhisiwi mtu yeyote kwenda uwanjani na silaha ya aina yoyote, isipokuwa baadhi ya vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawataka wapenzi na mashabiki wa soka kuwa wastaarabu na kushangilia kwa kuheshima kwa kuzingatia kanuni za uendeshaji wa soka. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawatakia heri ya Pasaka na michezo yote miwili kuwa na mafanikio kwa timu zetu za Simba na Yanga .