Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Jamii imeshauriwa kuacha matumizi holela ya dawa ili kulinda figo zao kwakuwa matumizi ya dawa hizo ni miongoni mwa sababu zinazochangia mtu kupata ugonjwa sugu wa figo na kuleta madhara mengine kiafya.
Ushauri huo umetolewa na Bingwa wa Magonjwa ya Figo Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, Dkt. Immaculate Goima katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani, ambapo amebainisha kuwa jamii imekuwa na tabia ya matumizi holela ya dawa ikiwemo zile za kutuliza maumivu pamoja na dawa zitokanazo na mitishamba.
“Matumizi yoyote ya dawa yanahitaji ushauri kutoka kwa wataalam, tuache tabia ya kununua na kutumia dawa kiholela pale tunapojisikia maumivu au kuhisi changamoto yoyote kwenye mwili bali tufike katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu”.
Dkt. Goima ameongeza kuwa, wananchi wanatakiwa kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kujua afya ya figo zao na endapo watabainika kuwa na changamoto yoyote waweze kupatiwa matibabu mapema kabla figo zao hazijaathirika kwa kiwango kikubwa.
Siku ya Figo Duniani huadhimishwa alhamisi ya pili ya mwezi Machi kila mwaka ambapo kauli mbiu mwaka huu ni “Je! Figo zako ni salama, Jitambue mapema, linda afya ya figo”. Kauli mbiu hii inahamasisha jamii kufanya uchunguzi wa figo zao mapema na kupata matibabu kwa wale waliothirika na kuanza matibabu mapema ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
More Stories
NaCoNGO yazindua kikosi kazi cha ukusanyaji maoni
Dkt.Biteko awasili Barbados kunadi nishati safi kimataifa
Rais Dkt.Samia afanya uteuzi wa viongozi mbalimbali