December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yaombwa kufichua wanaobaka, kulawiti watoto

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

JAMII Mkoani Tabora imetakiwa kufichua wanaolaghai watoto wa kiume na kike na kuwafanyia vitendo vya ukatili ikiwemo kuwalawiti ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Uyui Zakaria Mwansasu alipokuwa akiongea na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii na wanafamilia katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini hapa.

Alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ulawiti, ubakaji na unyanyapaa miongoni mwa jamii vimekuwa vikiongezeka pasipo wahusika kuchukuliwa hatua yoyote licha ya kujulikana.

‘Unakuta mtoto anabakwa au kulawitiwa ila baada ya kesi kufikishwa katika vyombo vya utoaji haki, wahanga na hususani ndugu au jamaa wa karibu wanagoma kuja kutoa ushahidi, hili sio sahihi’, alisema.

Mwansasu alifafanua kuwa familia bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mmomonyoko wa maadili na vitendo vya ukatili wa kimwili, ambavyo havikubaliki.

Ili kukabiliana na changamoto hizo alisisitiza wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kujenga utamaduni wa kutoa taarifa punde tu wanapoona matukio ya namna hiyo, hii itasaidia ili kujenga familia bora zenye maadili ya Kitanzania.

Aliongeza kuwa serikali imeanzisha Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto 2021/2022 hadi 2025/2026 ambayo tayari inatekelezwa ikiwemo kuundwa madawati ya jinsia katika vituo vya polisi vyote.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoani hapa Panin Kerika aliikumbusha jamii kutimiza wajibu wao kwa watoto kama wazazi au walezi ikiwemo kuwajali, kuwalinda dhidi ya ukatili na kuzungumza nao mara kwa mara ili kufahamu changamoto zao.

Alibainisha kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ya ‘Imarisha  Maadili na Upendo kwa Familia Imara’, inazikumbusha familia kuzingatia maadili mema ikiwemo kufichua wale wote wanaowafanyia ukatili wanawake na watoto.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Uyui Moses Pesha alieleza kuwa viongozi wenye maadili mema wanatokana na familia iliyojengwa katika upendo, amani na maadili mema, hivyo akasisitiza wazazi na walezi kujali familia zao.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa huo Abakos Kululetela aliitaka jamii kutonyanyapaa watoto wenye ulemavu ikiwemo kuwaficha, bali wapewe mahitaji yao ya msingi ikiwemo upendo na lishe bora.

Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mkoani Tabora Zakaria Mwansasu (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Uyui Moses Pesha ( wa kwanza kushoto), Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa Abakos Kululetela ( wa pili kushoto), Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Panin Kerika (aliyeketi kulia) na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii katika kilele cha maadhimisho ya siku ya familia duniani iliyofanyika Kimkoa jana katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini hapa. Picha na Allan Vicent.