January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Iringa kuwa kitovu cha Utalii Kusini mwa Tanzania

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) amesema Serikali ina mpango wa kuufanya mkoa wa Iringa kuwa kitovu cha Utalii katika mikoa ya ukanda wa kusini mwa Tanzania kupitia utekelezaji wa mradi wa Mradi wa Kusimamia na Kuendeleza Utalii Nyanda za Juu Kusini (REGROW).

Amesema hayo leo alipotembelea eneo la uwekezaji la mradi wa REGROW la Kihesa Kilolo mkoani Iringa.

“Kihesa Kilolo ni eneo ambalo litakuwa kitovu cha utalii na limetengwa na Serikali kwa ajili ya mradi wa REGROW wenye lengo la kutunza maliasili pamoja na kuendeleza utalii” Mhe. Masanja amefafanua.

Aidha, ameweka bayana kuwa lengo kuu la uwekezaji huo kukuza utalii kusini mwa Tanzania na kupunguza uwezekano wa watalii kuelemea upande wa Kaskazini mwa Tanzania hasa kipindi ambacho watalii wengi wanaingia nchini.

Amesema eneo hilo limetengwa kwa ajili ya miradi ya hoteli, viwanja vya golf, ofisi za Bodi ya Utalii Tanzania, uwekezaji wa mabenki na huduma zote muhimu.