November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

INEC inavyotoa elimu kuhusu Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

TUNAPOZUNGUMZIA Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni hatua za awali za mchakato wa uchaguzi. Uandikishaji huhusisha kuingiza majina na taarifa za watu waliotimiza sifa za kuwa wapiga kura kwenye orodha maalumu (daftari).

Elimu ya mpiga kura ni kumuwezesha mpiga kura kutekeleza kwa usahihi na kwa mujibu wa sheria, kanuni na utaratibu jukumu la msingi la kupiga kura ambalo linapatikana katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Uboreshaji ni mchakato wa kuingiza majina mapya ya watu waliotimiza sifa za kuwa wapiga kura, kuondoa majina ya watu waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura kutoka kwenye orodha ya awali na kurekebisha taarifa za wapiga kura ili waweze kupiga kura kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Kwa mujibu wa ibara ya 74(6xa) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1xa) cha sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya mwaka 2024. Tume ina jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na uchaguzi wa Madiwani kwa Tanzaia Bara.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akitoa mada katika semina ya Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali mkoa wa Dar es Salaam na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu Oboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025.Mkutano huo ulifanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam Juni 13 mwaka huu.

Kwa kuzingatia kifungu cha 16(5) cha sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya mwaka 2024, Tume ina wajibu wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya uchaguzi Mkuu uliomalizika na kabla ya siku ya uteuzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata.

Hata hivyo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaongozwa na Dira, Dhima. Dira ni uwepo wa mfumo wa uchaguzi unaoaminika na unaohakikisha uchaguzi huru na haki.

Dhima ni kusimami na kuratibu uendeshaji uchaguzi kwa kuzingatia sheria ili kuimarisha demokrasia kwa manufaa ya wananchi, vyama vya siasa na wagombea.

Kuelekea katika uchaguzi ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani, Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi imesema wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wataandikishwa katika daftari la kudumu la mpiga kura hata kama hawana kitambulisho cha NIDA.

Akizungumzia hilo wakati wa kikao kazi na Waandishi wa Habari hivi karibuni, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Giveness Aswile amesema kuwa na kadi ya NIDA sio kigezo cha kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali mkoa wa Dar es Salaam wakisikilza mada kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele alipokuwa akitoa elimu kuhusu Oboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani 2025

“Kuwa na kadi ya NIDA sio kigezo cha kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Wananchi wote wenye sifa wataandikishwa bila kujali kama wana kadi ya NIDA au la,” anasema Aswile.

Anasema, Mikutano hiyo ina lengo la kuwapa wadau taarifa za uwepo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwapitisha katika vifaa na mifumo ya uandikishaji pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni.

Aidha, ameyataja mambo yatakayohusika kwenye uboreshaji wa daftari kuwa ni pamoja na kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu 2025.

Lakini pia, kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walioandikishwa awali.

Vilevile, Kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania au kifo.

Hata hivyo kuna mifumo miwili ya kurahisisha maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua rasmi zoezi hilo Julai 01 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele uzinduzi huo utafanyika rasmi mkoani Kigoma.

Jaji Mwambegele amesema siku ya uzinduzi ndiyo siku ambayo uboreshaji utaanza katika Mkoa wa Kigoma, Katavi, Tabora, Kagera na Geita na baadaye mikoa mingine.

Ili kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, tume inatarajia kutekeleza zoezi hilo katika awamu ya kwanza kupitia mizunguko 13 kadri itakavyokuwa ikitoa ratiba.

Kupitia Mikutano na wadau mbalimbali iliyoanza Juni 7, mwaka huu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikikutana nao wakiwemo Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuwapa elimu kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wauhabarishe umma.

Hata hivyo Tume wamebainisha kuwa, katika Uboreshaji huo kutakuwa na mifumo miwili ukiwemo Mfumo Mkuu wa VRS (Voter Registration System) na Mfumo Saidizi wa OVRS (Online Voter Registration System).

VRS ni mfumo ambao umekuwa ukitumika katika mazoezi ya Uboreshaji wa Daftari uliotangulia ikiwemo mwaka 2015 na 2020.

Kuhusu, OVRS ni mfumo ambao Tume imeuanzisha kwa lengo la kurahisisha Utoaji huduma kwa Wananchi kwa njia ya Mtandao.

Kwa mujibu wa INEC, Mifumo yote miwili itahusisha Matumizi ya Fomu tatu za uandikishaji kama ilivyokuwa katika mazoezi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura miaka ya 2014/15 na 2019/20.

INEC imebainisha kuwa, Mifumo yote miwili inahusisha matumizi ya Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) ambayo huwa inatolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Aidha, Mifumo hiyo ya uandikishaji ya INEC inaweza kuvuta taarifa za NIDA iwapo mpiga kura atakuwa na NIN, hivyo kurahisisha zoezi la uandikishaji ingawa namba hiyo si hitaji la lazima ili mpiga kura kujiandikisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hauhusiani na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2024.

Kailima amesema, Waandishi wa Habari wana jukumu kubwa la kuelimisha wananchi na kuzuia kusambaa kwa taarifa za upotoshaji.

Taarifa kama ile inayodai kwamba uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unahusika na maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa jambo ambalo sio kweli.

Mkurugenzi huyo wa uchaguzi amenukuu kifungu cha 10(1) (c) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 ambacho kinaelekeza kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itasimamia uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutumia sheria itakayotungwa.

“Kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024 kinaweka sharti kwa Tume kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika Sheria itakayotungwa na Bunge. Sheria hiyo bado haijatungwa,” amesema Kailima.

Amewaasa watu wanofanya upotoshaji huo waache kwa kuwa matokeo yake ni mabaya na yanaweza kuathiri mwenendo wa kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Amesisitiza kuwa sheria mbili zilizofutwa ambazo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 hazihusiani na uchaguzi wa serikali za mitaa, hivyo wananchi wawe makini na wapotoshaji.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka aliwasilisha Mada kuhusu Maadili ya Utangazaji

Mhandisi Kisaka amesema katika kutekeleza wajibu wa vyombo vya utangazaji vinatakiwa kuzingatia mambo mbalimbali yakiwemo sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya utangazaji, Maadili na taaluma ya utangazaji.

Kingine cha kuzingatia ni kuhakikisha kuwa jitihada za kakusudi zinafanyika ili matangazo yaweze kufikika sehemu yote ya nchi ya Tanzania Bara ‘Public Broadcaster’.

Lakini pia, kutobagua kundi lolote pamoja na kuhakikisha kuwa kunakuwa na wakalimani wa lugha, kutumia lugha fasaha ya kiswahili ikiwa ni pamoja na matamshi sahihi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Patrick Kipangula akiwasilisha mada kuhusu maadili ya uandishi wa habari hasa wakati wa uchaguzi.

Kipangula amesema, vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kutoa taarifa za ukweli na sahihi kwa umma wakati wote wa uchaguzi. Kupotosha au kutoa taarifa zisizo sahihi kunaweza kusababisha hofu.

Aidha, amesema kuchochea ghasia na kupunguza imani ya wananchi kwa mchakato wa uchaguzi. Habari itaonekana ya ukweli iwapo hoja za tukio au suala husika linaeleweka kikamilifu.

Mmoja wa waandishi wa habari kutoka katika gazeti la majira, Penina Malundo amesema amejisikia furaha kupata elimu kuhusu Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwa ni kuna mambo mengi ambayo alikuwa hayatambui.

Amesema, yeye kama mwandishi wa habari atatumia vyema kalamu yake kuuhabarisha umma ili kila mtanzania atambue umuhimu wa kujihandikisha katika daftari hilo ili apate haki ya msingi ya kupiga kura.

“Nafurahi nimepata mafunzo haya kwa muda siku mbili nimejifunza mengi hivyo nitauhabarisha umma vizuri hasa kwa kutumia kalamu yangu kila mtanzania aweze kushiriki nyema katika kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura,” amesema Penina.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema imekamilisha maandalizi muhimu kwaajili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya uandikishaji vinavyojumuisha BVR Kits 6,000.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema BVR Kits hizo zitatumia vishkwambi kuchukua taarifa za wapiga kura ikiwemo picha, saini na alama za vidole.

“BVR Kits za sasa zinatumia mfumo endeshi wa android na uzito wake ni kilogramu 18, awali zilikuwa zinatumia mfumo endeshi wa window na uzito wa kilogramu 35,” amesema Kailima.

Amesema, Mfumo wa Uandikishaji wa Wapiga Kura (Voters Registration System-VRS) umefanyiwa usanifu na kuboreshwa ili kukidhi aina ya BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu endeshi ya android.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema, BRV Kits hizo zitakuwa rahisi kubeba na kufanya zoezi la Uboreshaji wa Daftari kuwa rahisi haswa kwenye maeneo ya Vijijini ambapo Watendaji hulazimika kubeba vifaa kwa umbali mrefu.

“Mfumo wa teknolojia hii ya BVR hutumika katika kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine. Uandikishaji huu wa wapiga kura utahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura,” amesema Jaji Jacobs.

Katika hatua nyingine Jaji Jacobs amesema waandishi wamekuwa kiungo kikubwa kupitia taarifa za habari, vipindi na makala katika kutoa elimu ya mpiga kura.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kuwafikia walengwa kote nchini ili waweze kupata taarifa ya nini wanapaswa kufanya kwa mustakabali wa Taifa.

“Tunawasihi muendelee kutuunganisha na wadau. Tume itaendelea kuweka milango wazi kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara,” amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema, wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu kujiandikisha na umuhimu wake, hivyo Tume imejikita katika kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa ili uboreshaji uwe wa mafanikio.

Hata hivyo amesema, mifumo yote miwili itahusisha fomu tatu, Namba moja, Kuandikisha wapiga kura wapya, Namba 5A wanaoboresha taarifa zao, wanaohama vituo, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, na namba 5B kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwepo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Uandikishaji wa wapiga kura utahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa Daftari wa mwaka 2024/2025 utatumia teknolojia ya BVR Kits zilizoboreshwa kwa kuwekewa program endeshi ya kisasa zaidi.

Amesema sambamba na mabadiliko ya Teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha Zoezi la uboreshaji wa Daftari,imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao Kwa mara ya kwanza utamwezesha mpiga kura aliyepo kwenye Daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo Kwa kutumia simu au kompyuta na baadae kutembelea kituo anachokusudia kujiandikisha Ili apatiwe kadi yake ya mpiga kura

Aidha Amesema kifungu Cha 9(1) na (2) Cha sheria ya uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani Na 1 ya Mwaka 2024 uboreshaji wa Daftari utahusu watu wote wenye sifa za kuandikishwa kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura

“Tume imeweka utaratibu Kwa watu wenye ulemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito na wakina mama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni kupewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni”Amesema Mwambegele

Aidha amebainisha kuwa Tume Chini ya kifungu Cha 10(1)(g) Cha sheria ya tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya mwaka 2024,imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchini

Hata hivyo amesema Katika kutekeleza jukumu hilo,imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa.wa kutosha Kuhusu uboreshaji huo

“Njia mbalimbali za kutoa elimu ya mpiga kura zitatumika Ili kuhakikisha kwamba wadau wote wanapata fursa ya kuelimisha na kuelewa mambo yote ya msingi Kuhusu uboreshaji huu ili wajitokeze Kwa wingi kushiriki kwenye Zoezi hilo,”. amesema Mwambegele.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, iliandaa mikutano mfululizo kwa wadau wake kauanzia Juni 07 hadi 15, 2024. Baadae Tume itafanya mikutano na wadau kwenye mikoa yote kwa kuzingatia ratiba ya uboreshaji wa Daftari.

Mikutano hiyo ina lengo la kuwapa wadau taarifa za uwepo wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwapitisha katika vifaa na mifumo ya uandikishaji pamoja na kuona namna zoezi litakavyofanyika vituoni.