Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imetumia kiasi cha milioni 90 katika utengenezaji wa madawati 1,245, kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi zilizopo katika halmashauri hiyo.
Madawati hayo yaliotengezezwa kwa fedha za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo yatapunguza changamoto ya uhaba wa madawati katika shule 24 za msingi ambapo wanafunzi 3,735 wanatarajiwa kutumia madawati hayo na kwa kila dawati watakaa wanafunzi watatu.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi madawati hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,iliofanyika shule ya msingi Mwenge iliopo Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Marco Isack amesema,mahitaji ya madawati katika shule za msingi ni madawati 27,153 yaliopo ni 19,995 huku pungufu ikiwa ni 7,158.
“Utengenezaji wa madawati umeenda na ujenzi wa vyumba 6 vipya vya madarasa,ukamilishaji wa vyumba 27 vya madarasa, matundu 6 ya vyoo,nyumba 1 ya walimu ambalo jumla ya milioni 327,127,850( zaidi ya milioni 327),zimetumika kutoka mapato ya ndani ya ya halmashauri ,sasa jumla ya zaidi ya milioni 417(417,127,850) la mapato ya ndani imetumika kujenga miundombinu na kutengeneza madawati katika idara ya elimu msingi,” amesema Isack.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, amesema hiyo ni awamu ya pili ya utoaji wa madawati hivyo baada ya miezi mitatu watatoa tena madawati 1,000, lengo ni kuwa mwezi wa Septemba suala la madawati libaki kuwa historia.
Hivyo kuelekeza nguvu katika maeneo mengine ikiwemo kukabiliana na changamoto ya nyumba za walimu na matundu ya vyoo ili watoto wapate sehemu ambazo zitafanana na mazingira ya utoaji wa elimu.
“Hadi sasa tuna upungufu wa madawati 7,000,tumedhamiria hadi kufikia Septemba mwaka huu tuwe tumemaliza changamoto ya madawati,nitoe rai kwa viongozi wenzangu na wazazi wote, tuendelee kuguswa na jambo hili,”amesema Masalla.
Naye Diwani wa Kata ya Nyamanoro, George Maganiko amesema shule ya msingi Mwenge inakabiliwa na uhaba wa ofisi ya walimu pia ameishukuru halmashauri hiyo kutoa madawati 155 katika shule hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza,Robert Gabriel ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Ilemela kwa utengenezaji wa madawati 1200 kwajili ya shule za msingi huku akiiagiza manispaa hiyo kuendelea kukusanya mapato ya ndani zaidi kwajili ya kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu.
More Stories
Mwalimu adaiwa kumfanyia ukatili mwanafunziÂ
NAOT watakiwa kuendana na viwango vya ukaguzi
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu