Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima,vyumba vya madarasa 110,vyenye thamani ya bilioni 2.2,fedha kutoka Serikali Kuu.
Ambapo vyumba hivyo ni kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 kupata nafasi ya kuanza masomo kwa wakati.
Na ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na kuwaondolea mzigo wazazi wa kuchangia ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi (watoto) wao wanaokuwa wanatarajia kuanza kidato cha kwanza kwa mwaka mpya wa masomo.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa madarasa 110, katika hafla ya makabidhiano ya madarasa hayo iliofanyika shule ya sekondari Bujingwa,wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Kiasi kilichopokelewa kwa ajili ya ujenzi na shughuli zilizofanywa
Mhandisi Modest, ameeleza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipokea kiasi cha bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 katika shule za sekondari 23, pamoja na seti za meza na viti 5,500 na ofisi tatu.
Nini lengo la ujenzi huo.
Mhandisi Modest, ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kuwezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023, kupata nafasi na kuanza masomo kwa wakati pamoja na kuwa na mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia.
Mahitaji ya vyumba vya madarasa
Ameeleza kuwa mahitaji ya vyumba vya madarasa ya kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 ni madarasa 252 kwa ajili ya wanafunzi 12,548 kati yao wasichana 6537 na wavulana 6011 huku vyumba vya madarasa vilivyokuwepo ni 142 na upungufu ni 110.
“Ukamilishaji wa mradi huu utakidhi mahitaji ya wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023,hadi Desemba 21,2022 shule zote zilizopokea fedha zimekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 vyenye seti ya viti na meza 5,500 na tumeweza kuongeza ofisi 3,”ameeleza Mhandisi Modest.
Ushiriki wa jamii katika mradi huo
Mhandisi Modest, ameeleza kuwa jamii pia ilishiriki katika mradi huo kwa kusaidia kutoa viashiria na nguvu kazi ambavyo vinakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya milioni 12, kama ishara ya kuunga juhudi ya serikali yao.
Mafanikio ya mradi huo.
Ameeleza kuwa kupitia mradi huo wanafunzi watapata mazingira bora ya kujifunzia na jamii pia imepata ujuzi wa namna bora wa kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
“Tumeweza kutoa ajira fupi kwa wananchi,1412,tumeweza kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,tumewezesha serikali kupata kodi kutoka kwa mafundi na wazabuni waliouza vifaa vyao katika ujenzi huo,”ameeleza Mhandisi Modest.
Changamoto katika mradi huo
Mhandisi Modest, ameeleza kuwa katika kipindi cha kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyumba 110 vya madarasa,wamekutana na changamoto ya kupanda kwa bei ya vifaa ghafla,kukatika kwa umeme na hupatikanaji wa maji,utatuzi wa migogoro ambapo ushirikishaji wa jamii ulisaidia hususani suala la upatikanaji wa maji kwa ajili ya ujenzi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuph Bujiku, ameeleza kuwa kama chama wameridhishwa na kazi iliofanywa ya ujenzi huo wa vyumba vya madarasa kwani viongozi wamehakikisha wanasimamia vyema.
Akitoa salamu za Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula,Katibu wa Mbunge huyo Kazungu Safari, ameeleza kuwa kipindi cha nyuma mwezi kama huu watendaji wa Kata na mitaa wangekuwa wanasumbuana na wananchi kuchangisha shilingi 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
“Tunamshukuru Rais kwa ubunifu wake na kutuletea kiasi cha bilioni 2.2,kazi imefanyika kwa muda mfupi lakini tungeendelea na utaratibu ule ule wa kuchangishana tungechelewa na kusubili sana,”ameeleza Kazungu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, ameeleza kuwa kazi ya ujenzi wa vyumba hivyo 110 vya madarasa wameifanya takribani siku 45 hadi 50.
“Wakati tunapewa fedha,tulipewa siku 75 katika siku hizo wiki mbili Ilemela sisi tulikuwa bado hatujaanza kazi kwa sababu za kimfumo tulichelewa,lakini tulianza maandalizi mengine na tulipo anza kulikuwa hakuna kusimama mpaka leo hii tunapokamilisha hii kazi,”ameeleza Massala.
Pia ameeleza kuwa,kuna takwimu ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa na wananchi lakini havijamaliziwa ni kubwa lakini kwa mwaka wa fedha ulio isha zaidi ya vyumba 126 walivifanyia kazi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.
“Kwa mwaka huku wa fedha tayari tumeisha tenga fedha ,kilichokuwa kimetukwamisha kwa sehemu kubwa ni umaliziaji wa vyumba hivi 110 lakini baada ya hapo bado tunakazi ya kumalizia madarasa yalionzishwa na jamii ikiwa ni kumuunga mkono Rais,”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza,Elikana Balandya ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza ulipatiwa kiasi cha bilioni 19.66,kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 983 kati ya hayo madarasa 110 yamejengwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
“Nawashukuru na kuwapongeza viongozi wote wa Ilemela kwa kuhakikisha madarasa yote yanajengwa na kukamilika kwa wakati,na hii inatuonesha kuwa wanafunzi waliochaguliwa shule itakapofunguliwa watajiunga na masomo,tushirikiane kuhakikisha watoto woliochaguliwa ifikapo Januari 9,2023 wanajiunga kwani hakuna jambo unaloweza kumpa mtoto zaidi ya elimu,na madarasa haya hayatokuwa na maana kama watoto hawatajiunga katika masomo,”.
Akizungumza mara baada ya kupokea vyumba hivyo vya madarasa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, ameeleza kuwa katika kupokea madarasa hayo ni mafanikio ya miaka miwili ya Rais ambapo mwaka jana pia walipokea madarasa kama hayo yaliotokana na fedha za uviko-19.
Ameeleza kuwa kwa wale wenye kumbukumbu kwa siku za mwisho za mwezi Desemba,wanajua kuwa kinakuwa ni kipindi kigumu sana cha kufukuziana,kukabana na kukasirikiana kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na uwenda yenyewe yangekuwa mawili au matatu.
“Katika Wilaya zote 7, za Mkoa wa Mwanza Ilemela mmewakanyaga wenzangu vibaya sana, wengine hata ukiwauliza nyie mnakabidhi lini madarasa lugha zinakuwa zinapiga chenga,hivyo Ilemela nawapongeza sana,”ameeleza Malima.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu