January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilemela yakabidhi vyumba vya madarasa fedha za Uviko- 19

Judith Ferdinand, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,amekabidhiwa jumla ya vyumba vya madarasa 92 vyenye thamani ya bilioni 1.84,kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambavyo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 kutokana na fedha za UVIKO-19.

Ambapo Halmashauri hiyo ilipokea jumla ya kiasi cha fedha bilioni 1.94 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 97 ambapo vyumba 5 vya madarasa katika shule ya sekondari Angeline Mabula vilichelewa kupata fedha hizo na hadi sasa vipo katika hatua ya ukamilishaji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kumkabidhi vyumba hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel iliofanyika shule ya sekondari Bujingwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Modest Apolinary amesema halmashauri hiyo ilipokea zaidi ya bilioni 1.9 huku changamoto walizokutana nazo wakati wa utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na kupanda kwa vifaa vya ujenzi.

Amesema,mbali na ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa pia katika mradi huo halmashauri imeongeza ujenzi wa ofisi ndogo za walimu 28 na kati ya ofisi hizo nne zina vyoo vya ndani.

Pia amesema, katika fedha hizo wamefanikiwa kutengeneza viti na meza 4,850 ambavyo vitatosha kwenye vyumba hivyo.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipangiwa jumla ya wanafunzi 600 watakaojiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2022.

“Ni mpango wa serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga na shule ya sekondari mwaka 2022 na madarasa yawe yamekamilika, kupitia usimamizi makini wa fedha tulizopewa tumebakiwa na ziada ya milioni 24,” amesema Apolnary.

Aidha amesema,awali halmashauri hiyo ilikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 114 tayari vyumba 97 vimekamilika na vingine 16 vilikuwepo,hivyokwa sasa hawana upungufu na wanafunzi wote waliopangwa watasoma bila kuwepo na changamoto hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel ameipongeza halmashauri hiyo kwa kwendana na muda wa ujenzi wa vyumba hivyo na kuvikabidhi na kuagiza halmashauri zingine zikajifunze wilayani humo.

Amesema majengo hayo yana ubora kwakuwa yamejengwa kwa kufuata hesababu za ujenzi, wametumia mbao ngumu za mkongo na kwenye vyumba hivyo wamefanya wiring na umeme umeshwekwa.

“Kwa ubora huu wa vyumba hivi vya madarasa hakuna haja ya kwenda kukodi ukumbi kwa ajili ya kufanyia mikutano, kila kitu kinaweza kumalizikia hukuhuku,”amesema Mhandisi Gabriel.

Amesema wilaya ya Ilemela imetoa tafsiri kwamba darasa moja linaweza kujengwa chini ya milioni 20

Amepongeza mafanikio hayo na kuitaka halmashauri kuyalinda ili kuendelea kufanya kazi zingine za maendeleo kwenye halmashauri hiyo.

Pia ameagiza viongozi kuhakikisha wanasimamia mipango yote ya kimaendeleo kwa kushirikiana na wataalam wa halmashauri hiyo na kuendeleza moyo wa kujitoa kwa viongozi na wananchi wote walioshiriki katika ujenzi miradi mingine ya maendeleo.

Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Lumala Angel Mussa amesema zamani wakati wanaenda kuanza masomo walipangiwa kwenda na vifaa vingi ikiwemo kiti na meza lakini kwa sasa serikali imewarahisishia na kuwapunguzia michango ambayo wangetakiwa kwenda nayo wanapoenda kuripoti.

Madarasa hayo yamejengwa kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa dhidi ya mapambano ya UVIKO-19.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,akikat utepe katika hafla ya kukabidhiwa vyumba 92 vya madarasa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, iliofanyika katika shule ya sekondari Bujingwa,ambapo madarasa hayo yamejengwa kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa dhidi ya mapambano ya UVIKO-19.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel,akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa vyumba 92 vya madarasa kati ya 97 na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, iliofanyika katika shule ya sekondari Bujingwa,ambapo madarasa hayo yamejengwa kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa dhidi ya mapambano ya UVIKO-19.
Muonekano wa ndani kati madarasa 92,aliyokabidhiwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,yaliyotekelezwa na fedha za UVIKO-19.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Modest Apolinary akizungumza wakati wa hafla ya kumkabidhi vyumba 92 vya madarasa kati ya 97,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel, iliofanyika shule ya sekondari Bujingwa wilayani Ilemela, ambapo madarasa hayo yamejengwa kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa dhidi ya mapambano ya UVIKO-19.