Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Timu ya Madiwani na wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha imefanya ziara katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela yenye lengo la kujifunza namna Halmashauri hiyo ilivyoweza kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kutoa matokeo chanya.
Ambapo miongoni mwa miradi iliyowavutia na kuwa chachu ya wao kutembelea Halmashauri hiyo na kujifunza ni pamoja na mradi wa stendi ya mabasi na maegesho ya malori Nyamh’ongolo.
Ugeni huo ulitembelea mradi wa stendi ya mabasi na maegesho ya malori Nyamh’ongolo uliogharimu kiasi cha zaidi ya bilioni 26 (26,649,749,438.00),ambapo stendi ya mabasi imegharimu kiasi cha zaidi ya bilioni 16(16,691,090,435.00).
Huku mradi wa maegesho ya malori umegharimu kiasi cha zaidi ya bilioni 8 (8,234,182,381.00) na gharama za Mtaalam Mshauri zaidi ya bilioni 1.7(1,724,476,622.00).
Akizungumza wakati wa kikao cha mapokezi ya timu hiyo ya Madiwani na wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha,Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Renatus Mulunga amepongeza uamuzi wa madiwani na wataalam hao kutembelea Ilemela kwa ajili ya kujifunza ni jambo la kutoa moyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary, ameeleza kwa ushirikiano mkubwa wa Madiwani inaendelea kuibua vyanzo mbalimbali vinavyoweza kuipatia halmashauri hiyo mapato pamoja na kuboresha usimamizi wa mapato na vyanzo vya mapato vilivyopo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Ojung’u Salekwa amepongeza juhudi kubwa inayooneka kwa vitendo kwa timu nzima ya Ilemela na kukiri wazi kuwa ipo dalili nzuri ya ushirikiano mzuri kati ya Madiwani na wataalam wa Ilemela.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha Selemani Msumi amepongeza kazi nzuri inayofanywa na wataalam na uongozi mzima wa Ilemela ambapo hadi sasa Manispaa ya Ilemela imekusanya asilimia 72 ya matarajio yake ya makusanyo kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023.
Mtaalam wa miradi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela James Wembe, ameeleza kuwa ni vizuri kushirikisha wataalam washauri wa ndani na nje ya Halmashauri husika kutoa mawazo yao katika masuala ya miradi inayotekelezwa eneo husika.
“Zipo hatua za kufuata katika kufanikisha miradi mikubwa kama hii , kuanzia mpango (planning) ,utekelezaji (Implementations) na kazi yenyewe (operations),”ameeleza Wembe.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi