Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Dodoma
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imeweza kuwasaidia wakulima wa alizeti kwa kuhamasisha kila kaya kulima zao hilo kuanzia ekari moja hadi tatu, nia ikiwa kuwawezesha kiuchumi, kwani zao hilo soko lake ni kubwa ndani na nje ya nchi.
Lakini pia halmashauri hiyo imeweza kuwasaidia kupata mbegu za alizeti za ruzuku kwa sh.5,000 kwa kilo moja badala ya sh.20,000 hivyo kutoa nafuu kubwa kwa wakulima, huku wakiweza pia kuwasambazia mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yalisemwa Agosti 6, 2024 na Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Gurisha Msemo wakati anazungumza na mwandishi wa habari kwenye Banda la Ikungi la Maonesho ya Nanenane ya kitaifa Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma.
Msemo amesema halmashauri hiyo wakulima wake wanategemea kilimo kwa shughuli zao za kupata kipato kwa asilimia 80 hadi 85, huku halmashauri hiyo kwa Mapato ya Ndani inategemea wakulima kwa asilimia 65, hivyo ndiyo maana wameweka mkazo kuwaendeleza wakulima hao ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya kilimo bora.
“Katika kuhakikisha zao la alizeti ndiyo linakuwa zao kuu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, kwanza tumeweza kufanya uhamasishaji wa msimu wa kilimo kwa kuhakikisha kila kaya angalau inalima ekari moja hadi tatu za alizeti. Lakini pamoja na hiyo, tumeweza kutoa elimu ya jinsi ya kulima alizeti kwa kutumia kanuni bora ya kilimo ambayo ndiyo itaweza kumtoa mkulima na kuweza kupata tija. Na tatu, tuweza kutoa mbegu bora yenye ruzuku ya Serikali ambayo ingembidi mkulima ainunue kwa sh. 20,000 kwa kilo, lakini kwa kupitia ruzuku ameinunua kwa sh. 5,000 kwa kilo.
“Hiyo ndiyo Rais Dkt. Samia ameweza kutusaidia katika Sekta ya Kilimo, hasa katika zao la alizeti kwenye wilaya yetu na mkoa wetu wa Singida. Lakini pia, tumeweza kusambaza mbolea ya ruzuku kwenye vijiji vyote 101 vilivyopo ndani ya kata 28 katika Wilaya ya Ikungi, ambapo asilimia 70 ya vijiji vilifikiwa na mbolea hiyo, ambapo tani 257 zimeweza kutumika kwenye wilaya yetu kwa msimu wa 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 88 ukilinganisha na msimu wa 2022/2023 ambao tulisambaza tani 36 tu” amesema Msemo.
Msemo amesema kwa kutumia mbegu ya ruzuku ambayo ilikuwa na ubora, na mbolea ya ruzuku, wakulima waliitikia na kuweza kulima kwa wingi na manufaa yake wameyaona.
Msemo amesema Wilaya ya Ikungi inategemea mazao makuu matatu ambayo ni alizeti ambalo ni zao kuu la biashara, kuna mtama ambalo ni zao kuu la chakula, na mbogamboga yaani vitunguu ambalo pia ni zao kuu la biashara, na katika nanenane hiyo wamekwenda kuonesha zao la alizeti, mtama na vitunguu. Na wameweza kulima alizeti hiyo iliyopandwa kwa mbegu ya kisasa kwenye Shamba Darasa. Pia wamepanda mtama na vitunguu.
“Kwenye Nanenane hii tumeweza kuonesha zao la alizeti ambalo ndiyo linampa mkulima fedha nyingi, na tumeonesha ukulima wa kisasa wa zao hili. Tumeonesha unaweza kuwa na mbegu mbalimbali za alizeti, na zikaonesha mafanikio kutokana na mazingira yetu, na katika kipando hiki cha alizeti tuna mbegu aina nne ambazo ni Sunbloom ambayo ni mbegu yenye ruzuku ya Serikali, na tuliweza kuletewa na tumewasambazia wakulima wetu ambao wameweza kuzalisha.
“Lakini tuna mbegu ya pili aina ya
Seedco LG, ambayo tumeweza kuionesha katika vipando hivi, na wakulima wamekuja kujifunza. Pia tuna mbegu ya Aguara 6 ambayo nayo ni mbegu chotara na inaweza kuhimili katika mazingira yetu, na nne ni Super Sun 66, nayo ni mbegu chotara ambayo ina uwezo wa kuzalisha mazao kwenye mazingira yetu. Hivyo katika maonesho haya ya nanenane, tumemuonesha mkulima namna anaweza kutumia mbegu hizo akapata manufaa” amesema Msemo.
Msemo amesema mkulima atakaetumia mbegu hizo za alizeti huku akifuata kanuni bora za kilimo atapata kati ya gunia 12 hadi 18 kwa ekari moja, na ataachana na kilimo cha mazoea ambacho kinampa gunia tatu hadi tano kwa ekari moja, na wakulima wengi wa Ikungi wameanza kubadilika, na wameanza kutumia mbegu bora, ambapo zamani walikuwa wanatumia nafaka, mazao waliyozalisha ndiyo wanafanya mbegu.
“Kwa kutumia mazao waliyolima kuwa mbegu, uzalishaji ulikuwa unadumaa mwaka hadi mwaka, lakini kwa sasa uzalishaji unaongezeka mwaka hadi mwaka, lakini kwa sasa uzaliahaji kwenye wilaya yetu umeongezeka kwa kipindi hiki cha miaka mitatu. Cha kwanza kabisa ni baada ya Serikali kuanza kutoa mbegu ya ruzuku, ambapo mwaka 2021/2022 tuliweza kupokea mbegu ya ruzuku tani 35, msimu wa 2022/2023 tulipokea mbegu ya ruzuku tani 77.
“Na uzalishaji wetu uliongezeka kutoka tani 26 hadi tani 74 kwa msimu huo wa 2922/2023, na sasa tupo kwenye mavuno kwa asilimia 70, na tuna mategemeo ya kuvuna mavuno tani 84 ya zao la alizeti, mpaka sasa hivi tunavyoongea, wakulima wameshavuna kwa asilimia 76 takribani tani 58, na wameanza kuuza na bei bado ni nzuri” amesema Msemo.
Naye mkulima wa alizeti kutoka Wilaya ya Ikungi ambaye alikwenda kwenye Maonesho ya Nanenane Dodoma kuonesha bidhaa zake, Asia Gudo, amesema alizeti imemkomboa kimaisha, kwani anapata mahitaji yake ya msingi iikiwemo chakula, mavazi na malazi, huku akusomesha watoto wake, na hiyo ni kutokana na kuuza zao hilo kwa fedha nyingi kila msimu.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja