Na Lubango Mleka, Timesmajiraonline, Igunga
HALMASHAURI ya Wilaya ya Igunga imeanzisha kampeni ya kupambana na uharibifu wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya majiko ya gesi iitwayo Igunga pika na Mama Samia ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuachana na nishati chafu aliyoizindua miezi mitatu iliyopita.
Katika kampeni hiyo baadhi ya wakazi wa Kata ya Igunga, wamepewa majiko yanayotumia gesi na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ikiwa ni kampeni ya kupambana na uharibifu wa mazingira na kuhamasisha matumizi ya majiko hayo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Selwa Abdallah Hamid, alisema kuwa huo ni mwanzo kwa Halmashauri hiyo ambayo ina lengo la kuhakikisha wakazi wake wanatumia majiko hayo na kupiga vita uharibifu wa mazingira.
“Tunamuunga mkono Rais wetu kwa kuanzisha kampeni hii ambayo inalenga kutunza mazingira na kuhamasisha matumizi ya nishati safi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alieleza kuwa wameanza na Kata tano kati ya Kata 35 zilizopo Halmashauri hiyo kama kichocheo kwa kata zingine. Kata hizo ni Mwashiku, Nkinga, Igunga, Kining’inila na Mbutu.
Alisema kadri uwezo utakavyokuwa na Kata zingine nazo zitaongezwa ambapo wanataka asilimia 80 ya wakazi wa Halmashauri hiyo wawe wameachana na nishati chafu baada ya miaka kumi ijayo.
Katika kampeni hiyo kila kata katika kata tano zilizochaguliwa, wakazi wake kumi walipata majiko hayo bure baada ya kutimiza vigezo vilivyowekwa.
Mchumi wa Halmashsuri hiyo, Shaibu Dadi, alieleza kwamba nishati chafu mbali ya kuharibu mazingira pia inahatarisha afya za watumiaji na kuwa kampeni hiyo italinda afya zao.
Alieleza kuwa kumekuwa na matumizi makubwa ya kuni na mkaa na kuhatarisha mazingira na hivyo kukaribisha jangwa na ndio maana wanahamasisha kampeni hiyo kulinda mazingira.
“Wananchi tujitahidi sana kulinda mazingira na kuachana na matumizi ya nishati chafu kwa manufaa ya mazingira yetu na afya zetu.” Alisema.
Wakazi walionufaika na majiko hayo wanapongeza kampeni hiyo wakisema watatumia muda mfupi kupika na kufanya shughuli zingine huku wakiokoa muda wa kutafuta kuni.
“Tunapongeza sana kampeni hii ambayo italinda mazingira na afya zetu na kupata muda zaidi wa kufanya kazi zingine,” alieleza Veronica Lema.
Aidha Mwajuma Shabani alisema majiko hayo ya gesi yataondoa mauaji ya vikongwe kwa kuwa matumizi ya kuni yalikuwa yanasababisha akina mama kuwa na macho mekundu kutokana na moshi.
“Kwa kweli sasa hivi majiko ya gesi yataondoa kabisa mauaji ya vikongwe kwa vile majiko haya hayana moshi kama kuni na mkaa.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa