December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge,Uratibu ,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama akiwajulia hali majeruhi wa ajali ya Treni iliyotokea Bahi mwishoni mwa wiki iliyopita katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.

Idara ya maafa kuja na sera, muongozo kukabili majanga

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge,Uratibu ,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu ,Jenista Mhagama amesema,ofisi hiyo kupita idara ya maafa inaendelea kujipanga na kutengeneza sera na muongozo katika kukabiliana  na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza nchini.

Mhagama ametoa kauli hiyo leo alipotembelea hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma ili kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya treni iliyotokea wilayani Bahi  mwishoni mwa wiki iliyopita.

Amesema maboresho hayo yatawezesha idara hiyo  Kuokoa maisha ya watu na mali zao pindi majanga yanapotokea.

Aidha amesema ,uwekezaji ambao umefanywa na serikali mpaka sasa katika kuboresha huduma mbalimbali za Afya  nchini ,umekuwa  wa kuridhisha kutokana na huduma zinazotolewa katika hospitali za mikoa nchini.

“Huduma zilizotolewa katika hospitali yetu ya rufaa ya mkoa wa Dodoma imekuwa ni nzuri kama mlivyopata taarifa kwamba wagonjwa wote wametibiwa hapa na kuruhusiwa ” amesema Mhagama na kuongeza kuwa

“Serikali imeratibu vyema kuokoa maisha ya watanzania lakini pia imehakikisha walionusurika na ajali hii ya treni wameendelea kuwa salama.”amesema

Akitoa taarifa hospitalini hapo mbele ya Mhagama,Mkuu wa wilaya ya Dodoma,Josephat Maganga amesema walionusurika katika ajali hiyo walipatiwa usafiri na kuendelea na safari.

Awali Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Dodoma Ibenzi Ernest amesema kati ya majeruhi 66 wa ajali hiyo hadi asubuhi ya leo walikuwa wamebakia majeruhi wa tatu ambao wamesharuhusiwa kutoka na na hali zao kuimarika .

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRC) Peter Mathew amesema majeruhi wote wamehudumiwa ikiwa ni pamoja na kuwatafutia usafiri mingine kuendelea na safari.

Januari 2,mwaka huu,ilitokea ajali ya treni wilayani Bahi mkoani Dodoma ambayo ilisababisha vifo vya watu wa tatu na majeruhi 66 ambao wote wameshatibiwa na kuruhusiwa.