Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
KATIBU Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ameelekeza Menejimenti ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji ili kuchochea uchumi na fursa za ajira nchini.
Mhandisi Luhemeja amesema hayo, alipofanya ziara ya kiutendaji katika Ofisi ndogo za Makao Makuu ya PSSSF, jijini Dar es Salaam, ambapo, pamoja na kujionea shughuli za utoaji huduma, pia alipata fursa ya kuzungumza na Menejimengti ya Mfuko huo ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, CPA. Hosea Kashimba.
“Kuna kundi la vijana, kundi ambalo halina matumaini, zamani wahitimu wa chuo kikuu walikutana na ajira, lakini sasa hivi hali hiyo ni tofauti kidogo.” Alifafanua.
Alisema, PSSSF ni Mfuko mkubwa, hivyo una jukumu la kuwasaidia wastaafu, lakini pia kujenga mazingira ya kuwawezesha wastaafu wengi siku za usoni.
“Fungueni viwanda vingi, vitasaidia kutengeneza ajira kwa vijana, unaposaidia watu wengi na wewe unajisaidia.” Alifafanua.
Pia ameelekeza Menejimenti ya PSSSF, kuendelea kutoa elimu kwa umma, ili wananchi waweze kufahamu kazi kubwa ambayo imefanyika toka kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF, PPF, GEPF na LAPF na kuanzishwa PSSSF.
“Kazi kubwa na nzuri imefanyika kwa kipindi cha miaka mitano toka kuunganishwa kwa Mifuko, utendaji umeboreshwa kwa kiasi kikubwa, ni muhimu watanzania waweze kuelewa kazi ambayo Serikali inafanya kwa niaba yao” alisema Mhandisi Luhemeja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, amesema, yeye na Menejimenti yake kwa ujumla wameyapokea maelekezo hayo na ameahidi kuyafanyia kazi.
“Tayari tumewekeza kwenye maeneo ya uzalishaji ya viwanda, tumewekeza kwenye Machinjio ya kisasa, Nguru, kule Mvomero, Mkoani Morogoro, kiwanda cha Kuchakata Tangawizi, Mamba Miamba kilichoko Wilayani Same, Mkoani Kilimanjaro, kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi, Kilimanjaro (KLIC), kilichoko mjini Moshi na Kiwanda cha Chai Mponde, kilichoko Wilayani Lushoto Mkoani Tanga, na kama aivyoelekeza Katibu Mkuu, wetu, tufanye utafiti wa kina, ili kuendelea kuwekeza katika maeneo mengi zaidi na hivyo tutakuwa tumetimiza azma ya serikali ya kuzalisha ajira nyingi zaidi kwa watanzania.”Alisema CPA, Kashimba.
Aidha CPA. Kashimba amebainisha kuwa tokea kuunganishwa kwa Mifuko, uhai wa PSSSF sasa unaonekana, kwani Mfuko umeweza kulipa madeni yote iliyorithi toka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya awali.
“Ukuaji wa Mfuko umefikia kiasi cha trillioni 8, lakini pia gharama ya uendeshaji imepungua kwa asilimia 50 na hivyo tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha na kwakweli, jambo ambalo limeboresha utendaji kiasi kikubwa” alisema, CPA Hosea Kashimba.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja (kushoto) akizungumza na Menejimenti ya PSSSF, ikiongozwa na Mkurugenzi wake Mkuu, CPA. Hosea Kashimba (kulia)
Mhandisi Luhemeja, akizungumza na Menejimenti ya PSSSF
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja (katika), akiwa na Mkurugenzi Mkuu, PSSSF, CPA. Hosea Kashimba (kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Paul Kijazi.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, akipoewa maelezo ya kiutendaji ya huduma kwa wateja, kutoka kwa msimamizi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, PSSSF, Ilala, Bi. Mathilda Nyallu. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, akipokea mkoba wenye taarifa mbalimbali za kiutendaji za Mfuko, kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian (katikati waliokaa), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Frank Kilimba (wakwanza kushoto waliokaa), Mkurugenzi Mkuu PSSSF, CPA. Hosea Kashimba 9wakwanza kulia waliokaa), wakiwa katika picha ya pamoja na Menejiment ya PSSSF.
More Stories
Rukwa waanzisha utalii wa nyuki
Mhandisi Kundo ataka vyanzo vya maji vitunzwe
Dkt.Kazungu:Megawati 30 za Jotoardhi kuingia kwenye gridi ifikapo 2026/27