Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu Abdallah Shaibu Kaim amezindua huduma ya usafishaji figo kwa njia ya kuchuja damu (dialysis) katika Hospitali ya Malolo iliyopo katika halmashauri ya manispaa Tabora.
Akizungumza baada ya kutembelea na kujionea mitambo ya kutolea huduma hiyo, Shaib alipongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa uwekezaji mkubwa waliofanya ili kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.
Alipongeza uwekezaji mzuri wa hospitali hiyo katika manispaa hiyo na kuboresha huduma zake kwa wananchi ikiwemo kuanza kutoa huduma ya usafishaji figo na kuajiri wataalamu wa kutosha wa kutoa huduma mbalimbali za afya.
Shaibu alibainisha kuwa sekta binafsi zina mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla hivyo akatoa wito kwa wawekezaji wengine kuiga mfano huo.
‘Nawapongeza sana Hospitali ya Malolo kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya ikiwemo kuanza kutoa huduma hii ya uchujaji damu’, alisema.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo Mariam Karatta alisema mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umegharimu zaidi ya sh bil 1 na unaweza kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 48 kwa saa.
Alibainisha kuwa wamejipanga vizuri kutoa huduma hiyo kwa jamii na tayari wana wataalamu waliobobea wa usafishaji figo akiwemo daktari bingwa ya magonjwa ya figo, daktari wa uchujaji damu (dialysis) na wauguzi wa kutosha.
Katika kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatekelezwa kwa vitendo alisema wamejipanga vizuri kutoa huduma bora zaidi ikiwemo kuajiri Wataalamu wa Lishe, Maabara, Mionzi, Wafamasia na Vifaa tiba.
Alisema huduma hiyo ni mkombozi kwa wana Tabora na jamii kwa ujumla kwa kuwa wagonjwa wengi wenye tatizo hilo walikuwa wanalazimika kwenda DSM, Mwanza, Dodoma na Mikoa mingine yenye hospitali kubwa kufuata huduma hiyo.
Bi Mariam alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa sekta binafsi kufanya kazi na kutoa huduma bora za afya.
More Stories
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima